Wednesday 22 April 2015

Hali ya mazingira inatisha- Dk. Bilal


NA MWANDISHI WETU 
UHARIBIFU wa mazingira nchini umezidi kuongezeka hivyo kutishia kutoweka kwa rasilimali na viumbe hai muhimu na kuchochea ongezeko la umasikini.  
Miongoni mwa athari za uharibifu huo wa mazingira ni kuwepo kwa athari kubwa kwa sekta tegemeo kwa uchumi wa nchi na maisha ya binadamu kama kilimo, uvuvi, utalii na madini.
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Pili ya Hali ya Mazingira nchini, uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema Tanzania ikiwa moja ya nchi zinazoendelea, imekumbwa na uharibifu mkubwa wa mazingira na kwamba hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la umasikini. 
“Kuna uhusiano mkubwa kati ya uharibifu wa mazingira na umasikini. Kadri hali ya umasikini inavyoongezeka, ndivyo pia uharibifu wa mazingira unavyoongezeka,” alisema.
Dk. Bilal alisema ripoti hiyo inaonyesha kwamba ongezeko la uharibifu wa mazingira nchini linatokana na kuendelea kufyekwa kwa misitu, kuharibiwa kwa vyanzo vya maji, uchomaji moto na kuzagaa kwa taka ngumu. 
Sababu zingine, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni uchafuzi wa maji unaotokana na utiririshaji wa maji machafu ya viwandani na nyumbani na upotevu wa baioanuai.
Mbali na sababu hizo, Dk. Bilal alisema ongezeko la hali hiyo linaashiria kuwepo kwa upungufu katika kubuni, kutekeleza na kusimamia sheria, kanuni, mikakati na programu zilizowekwa kwa ajili ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira. 
Kutokana na hali hiyo, Makamu wa Rais aliziagiza taasisi za serikali na wadau kuhakikisha mazingira yanalindwa na wakati huo huo hatua kali zinachukuliwa dhidi ya watu wanaohusika na uharibifu wa mazingira. 
“Mazingira ni mhimili wa sekta za uzalishaji kama vile kilimo, utalii, uvuvi na madini. Changamoto iliyopo ni kuhakikisha mazingira na maliasili zetu zinatumika katika njia endelevu kwa kuzingatia uwiano mzuri kati ya matumizi ya rasilimali,” alisema.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mhandisi Dk. Binilith Mahenge, alisema kila mwaka nchini takriban hekta 400,000 za misitu zimekuwa zikipotea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati ya kuni na mkaa. 
Sambamba na hilo, Dk. Mahenge alisema kati ya mwaka 2000 na 2011 kumekuwa na ongezeko la matukio ya uchomaji moto ambapo yaliyoripotiwa ni 1,123,000. Matukio hayo yameripotiwa katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Tabora, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Morogoro. 
Pia, alisema uharibifu wa mazingira unachangiwa na ukosefu wa miundombinu ya majitaka katika miji mikubwa. 
Alisema asilimia 50 ya miji mkubwa nchini ina mifumo ya majitaka, ambayo hata hivyo haitoshelezi kwa kuwa inahudumia asilimia nane tu ya wakazi wa maeneo hayo.
Akitoa neno la shukrani, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema ripoti hiyo imewazindua wadau wengi, hivyo ni wajibu wa kila sekta kuhakikisha suala la mazingira linapewa kipaumbele. 
Alisema ni wazi kwamba uharibifu wa mazingira na umasikini ni chanda na pete hivyo jitihada za maskusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda mazingira kwa lengo la kuoresha maisha wa binadamu na viumbe hai.
“Suala la usimamizi wa sheria, sera, kanuni, taratibu na programu za hifadhi ya mazingira ni suala ambalo halina mjadala. Hatuna budi kuzisimamia ili kulinda mazingira na wakati huo huo kuchukua hatua hali dhidi ya wanaoharibu mazingira,” alisema. 
Nyalandu alisema ili kuhakikisha kunakuwa na usimamizi bora wa mazingira, sheria na sera zilizopo hazina budi kufanyiwa mabadiliko na kutoa adhabu kubwa kwa wale wanaokiuka.
Hafla hiyo ya uzinduzi ilihudhuriwa pia na mawaziri Samuel Sitta (Uchukuzi), Profesa Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais-Kazi Maalumu), Samia Suluhu Hassan (Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano) na Naibu Waziri Ofisi ya makamu wa Rais (Mazingira), Stephen Masele.
Pia walikuwepo makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali, wakurugenzi wa wizara na washirika wa maendeleo wakiwemo kutoka mashirika ya maendeleo ya Canada (CIDA) na Denmark (DANIDA).

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru