NA LATIFA GANZEL, MOROGORO
WATU watano wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma ya kukutwa na vipande vinane vya meno ya tembo, vikiwa vimevificha kwenye dumu la mafuta.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alisema tukio hilo lilitokea jana, saa 2:30 usiku katika eneo la Daraja Mbili, barabara ya kwenda Mikumi wilayani Kilosa.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa na polisi kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori, waliokuwa kwenye doria.
Paul alisema watu hao walichukua dumu la lita 20 la mafuta na kulipasua na kwamba ndani yake waliingiza vipande vya meno ya tembo na kuvipakia kwenye gari la mizigo aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 770 ABG.
Alisema gari hilo lilikuwa limepakia shehena ya pumba na kreti za soda, ambapo dumu hilo liliwekwa katikati.
Paul aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mohamed Juma (48) mkazi wa Mtawala Morogoro, Juma Athuman (35) mkazi wa Kiberege na Said Salum (23) ambaye ni utingo wa Fuso na mkazi wa Morogoro.
Wengine ni Omary Marumbo (26) mkazi wa Morogoro na Victoria Festo (43), ambaye ni mfanyabiashara na mwenye mzigo wa pumba iliyokuwa kwenye gari hilo.
Alisema watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.
Tuesday, 14 April 2015
Wanaswa na meno ya tembo
08:20
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru