Tuesday, 7 April 2015

Dk. Mhita afariki duniaNA MWANDISHI WETU
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA),Dk. Mohamed Mhita, amefariki dunia.
Dk. Mhita ambaye pia ni mume wa Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Zabein Mhita, anatarajiwa kuzikwa leo baada ya kuwasili kwa mkewe, aliyeko India kwa matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari, mtoto wa marehemu, Muhaji Mhita alisema baba yake aliugua maralia, Jumatatu alfajiri na kupelekwa hospitali, ambapo alifariki usiku.
Alisema walipofika hospitali walibaini kuwa shinikizo la damu lilikuwa juu  na alikutwsa na mauti saa nne usiku.
Muhaji alisema Jumapili usiku, baba yake alimjulisha juu ya hali yake,  ndipo  ilipofika alfajiri aliamua kumpeleka hospitali.

“Baba atazikwa kesho (leo), ila bado hatujapanga kama tutamzika Handeni au hapa Dar es Salaam, kwani tunamsubiri mama ambaye yuko nje ya nchi na leo (jana), usiku atakuwa ameshafika,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mboni Mhita, ambaye ni mtoto wa marehemu alisema amesikitishwa na kifo cha baba yake na kimewaachia simanzi kubwa.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, akizungumza na Uhuru kuhusiana na kifo hicho, alisema ni pigo kwa taifa kwa sababu bado lilikuwa linahitaji mchango wake.
Alisema licha ya Dk. Mhita kustaafu utumishi wa umma, walikuwa wakishirikiana naye katika mambo mbalimbali, ikiwemo ushauri na maelekezo kwa watumishi wa mamlaka.

“Tulishirikiana naye sana, kutokana na uzoefu wake muda wote wa utumishi wake wa mafanikio hapa TMA, hivyo tulikuwa tunatafuta mafanikio hayo pia kupitia yeye,” alisema.

Dk. Agnes ambaye alipokea kijiti kutoka kwa Dk. Mhita kuiongoza TMA, alitoa pole kwa familia na Watanzania kwa ujumla kutokana na msiba huo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru