Tuesday 7 April 2015

Jeshi la Zimamoto lawakumbuka yatima



NA MWANDISHI WETU, IRINGA 


JESHI la Zimamoto na Uokoaji mkoani Iringa, limetoa misaada mbalimbali kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Sister Theresia, kilichoko Tosamaganga, mkoani hapa.
Akikabidhi msaada huo, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto mkoani hapa, Kennedy Komba, alisema lengo la kutoa msaada huo ni kuwa karibu na jamii.
Alisema misaada hiyo itawasaidia yatima walioko katika vituo mbalimbali mkoani hapa.
Komba alisema watoto yatima wanakabiliana changamoto nyingi katika kupata mahitaji muhimu ikiwemo chakula, afya na malazi, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuwasaidia, ili kuondokana na hali ya utegemezi.

“Tumeamua kugawa msaada huu kwa kuguswa na matatizo mbalimbali wanayokabiliana nao vituo vingi vya kulelea watoto hapa nchini katika harakati zetu za kuhahikisha watoto yatima wanapata mahitaji muhimu katika maisha yao ya kila siku,” alisema.
Alisema hivi sasa jeshi hilo linapanga kurudisha faida inayopata kila mwaka kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kusaidia watu wasiojiweza.
Komba alisema msaada uliotolewa ni pamoja na mchele kilo 50, mbuzi, mafuta ya kupikia, sabuni na kuwapatia kifaa cha kuzimia moto.
Alisema jeshihilo  litakuwa likitoa msaada wa aina hiyo kila mara, ili kujiweka karibu na jamii  na kutambua shughuli wanazofanya.
Kaimu Msimamizi wa kituo hicho, Winfrida Mhongole, alilishukuru jeshi  hilo kwa msaada huo na kuwataka wadau wengine wawe na moyo wa kujitolea kwa watoto yatima.
Alisema kituo hicho kina pokelea watoto kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo ya Iringa Mbeya, Njombe, Morogoro na Dar es Salaam.



Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru