NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya
CCM, Balozi Seif Ali Iddi, amesema Watanzania wanaoishi Zanzibar na Bara,
wataendelea kushirikiana kwa miaka mingi zaidi kutokana na mwingiliano wao wa
kidamu.
Balozi Seif Ali Iddi |
Alisema uwepo wa
ushirikiano huo ndio njia pekee itakayotoa fursa kwa Watanzania hao kusaidiana
katika kutatua changamoto zinazowakabili miongoni mwao na vizazi vyao.
Balozi Iddi ambaye pia ni
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alisema hayo wakati akizungumza katika
mkutano wa ujirani mwema kati ya wanachama
wa CCM na viongozi wa Mkoa wa Magharibi, Unguja na kutoka Kata ya Mtoni, Wilaya ya
Temeke, Dar es salaam.
Mkutano huo ulifanyika
katika Tawi la CCM, Mwanakwerekwe B, kufuatia ziara za ujirani mwema kati ya
pande hizo mbili.
Balozi Iddi alisema
hakuna kikundi wala mtu anayeweza kuung’oa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,
kutokana na historia yake kwa jinsi ulivyoimarika kwa miaka kadhaa
iliyopita.
Katika hatua
nyingine, Balozi Iddi aliwataka na
kuwaomba Watanzania wote kuiunga mkono katiba inayopendekezwa.
Balozi Iddi alisema
katiba inayopendekezwa ina muundo wa mfumo waserikali mbili, ambazo zitadumisha
muungano kwa miaka 50 ijayo.
Akizungumzia suala la
uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba, mwaka huu, Balozi Iddi
aliwataka wanachama wa CCM, kuheshimu maamuzi ya vikao vya chama wakati wa
kuteua wagombea.
Alisema ni vyema kwa
wanachama kukubali maamuzi yanayotolewa na chama kwa kuwaunga mkono wagombea
waliopendekezwa katika ngazi zote.
Katibu wa kamati ya
ujirani mwema, Muhidini Makame Ussi, alisema ujirani mwema kati ya Kata ya
Mtoni na Wilaya ya Dimani, ulianza mwaka 1995.
Ussi alisema ujirani
mwema huo unaojumuisha viongozi na wanachama wa chama wa pande hizo mbili.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru