Saturday, 18 April 2015

Atakiwa kukanusha kauli ya upotoshaji


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
CHAMA cha Maalbino Tanzania (TAS) mkoa wa Mbeya, kimemtaka Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mbeya mjini, John Mwambigija, kuwathitibitishia Watanzania kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinahusika na vifo vya watu wa jamii hiyo.
Katibu wa chama hicho mkoani hapa, William Simwali, alisema hayo jana wakati akizungumza na MZALENDO kuhusu kauli iliyotolewa na Mwambigija akiwa kwenye mkutano wa hadhara juu ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Simwali alisema ni jambo la ajabu kwa baadhi ya wanasiasa kugeuza na kutaka kuwadanganya watu kuwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yamekuwa yakitokea kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu jambo ambalo si sahihi.
Alisema hivi karibuni Mwambigija akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kiwira wilayani Rungwe, alisema mkakati wa kuuawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ni mkakati unaotengenezwa na CCM, jambo ambalo si kweli
ìKwa sababu mauaji haya yameanza kuanzia mwaka 2006 na yaliendelea hadi mwaka 2009, na hakukuwa na uchaguzi wowote. Yakaanza tena mwaka 2011/2015, hivyo ina maana Tanzania kila mwaka ni mwaka wa uchaguzi? î alihoji Simwali.
Aliongeza wanasiasa aina ya Mwambigija wanatakiwa wawe wanatafuta maneno ya maana ya kuzungumza mbele za watu, hasa kwenye majukwaa ya kisiasa na siyo kutaka umaarufu kwa kuwaaminisha watanzania, mambo ambayo hayapo na kumtaka kukanusha kauli aliyotoa au kuelezea ukweli wake.
Kwa mujibu wa Simwali, hatu hiyo ya Mwambigija kusema jukwaani kuwa CCM ndiyo inayoua maalbino kwanza ni kukitendea dhambi Chama hicho.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru