Tuesday, 7 April 2015

Kardinali Pengo aweka msimamo


 • Aonya matukio ya ugaidi si mambo ya dini
 • Awataka wanaoamini wasambaze ujumbe


  NA MWANDISHI WETU

  ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema msimamo wake kuhusu katiba inayopendekezwa, uko pale pale na ametaka wanaoamini alichosema, wasambaze ujumbe wake kwa wengine.

  Muadhama Polycarp Kardinali Pengo
  Akizungumza na Chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), hivi karibuni, Askofu Pengo alitoa wito kwa waumini kuachwa huru wafanyeuamuzi kuipigia kura ya ndiyo au hapana  katiba hiyo, badala ya kushinikizwa na viongozi wa dini.
  Aidha, alisema kamwe hawezi kubadili kile alichosema, kwani ni ukweli anaouamini na alishaweka hilo wazi.

  Askofu Pengo alisema hayo jana, wakati wa ibada Maalumu ya Shirikisho la Kwaya Katoliki (SHIKWAKA), iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Kipawa, jijini Dar es Salaam, ambako kwaya zaidi ya 100 zilishiriki.


  “Jana (juzi), baada ya ibada kule Kurasini, walikuja waandishi wa habari na tukaanza kujadiliana na baadaye nilipomaliza wengine kisirisiri walijadili kwa nini sikusema chochote kuhusu katiba inayopendekezwa, sasa ndugu zangu niseme mara ngapi?” alihoji.


  “ Hivi ni nani anaweza kufikiria naweza kubadili maneno niliyosema, leo niseme kweli na kesho hapana. Nitakuwa mtu wa aina gani wa kubadili maneno na misimamo,”alisema.

  Alifafanua kuwa alishasema ukweli anaoujua, hivyo hana sababu ya kuurudia na kwamba kufanya hivyo ni kutafuta ugomvi.

  "Yale niliyosema kuhusu suala hilo nimesema mara moja na ni mara moja tu basi,’’ alisisitiza.

  Askofu Pengo aliwataka waumini na wasio waumini waliomsikia na kukubaliana na aliyosema, kuwa ni wakati wao kuendeleza taarifa hiyo kwa kusambaza  sehemu mbalimbali.

  Akirejea habari za kufufuka kwa Yesu, alisema kusambaza msimamo wake kutaenea kwa watu wengi zaidi, kwani ndivyo injili ya ufufuko wa Bwana Yesu ilivyoenea kwa Petro, ambaye awali wakati wa mateso ya Yesu, alimkana, lakinibaada ya kufufuka alisambaza taarifa hizo.

  Askofu Pengo alisema mashemasi kama Filipo,Stephano na wengine, hawakumwachia Petro kusambaza ufufuko wa Bwana Yesu, ila kila walipokwenda walitamka kuhusu ufufuko na hakukuwa na haja ya kumwita Petro kuelezea ufufuko huo.

  Alisema wasingefanya hivyo injili isingefika duniani kote.

  “Hivyo hivyo, wale walioamini niliyosema kuhusu msimamo wangu wa katiba inayopendekezwa, waendelee kusambaza kila wanapokwenda kwa manufaa ya nchi,” alisisitiza.

  Alisema ndivyo inayofundishwa na fumbo la ufufuko wake Yesu kuwa jambo jema halitegemei mtu mmoja kurudia rudia, kwani atakera watu.
  Askofu Pengo alisema anapoongelea tamko lake kuhusu katiba si kwamba, anataka kugeuza nafasi ya ibada kuwa mahali pa kutangaza siasa au shughuli za kijamii, bali neno lolote analofanya ni ukweli wake na hatobadili.

  Alitaka waumini kusimama na kusema potelea mbali katika kusimamia ukweli wa kile wanachoamini kwa kuwa jasiri bila kuogopa.
  Vitendo vya ugaidi

  Aidha, Pengo alizungumzia tukio la ugaidi nchini Kenya, lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 147 na kusema hakuna aliyefikiria kuwa  nchi hiyo  inaweza siku moja kuzingirwa na watu na kufanyika mauaji yenye msimamo wa imani za dini.

  Alisema ingawa nchi hiyo ilikuwa na malumbano kadhaa, lakini si dini. Alisema tukio hilo halipendezi si kwa Waislamu wala Wakristo.


  “Tumwombe Kristo atuponye na kutuepusha na balaa hilo na yasiendelee kutokea kwa jirani zetu, huku kila mmoja akihakikisha kuwa na ujasiri wa kubaki na msimamo wetu,’’ alisema.

  Waraka wa maaskofu
                      
  Mwezi uliopita, Askofu Pengo wakati akifungua mafungo ya WAWATA, yaliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam, alikosoa waraka wa maaskofu kupitia Jukwaa la Kikristo, uliotaka waumini kupiga kura ya hapana kwa katiba inayopendekezwa.

  Alisema kuwaamulia ni kuwadharau kuwa hawana uwezo wa kufanya uamuzi  sahihi.
  Awali, Jukwaa la Wakristo Tanzania liliwataka waumini wake kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma katiba inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya hapana.

  Taarifa hiyo ilitiwa saini na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk. Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.

  Waliompinga Pengo

  Baada ya Askofu Pengo kutoa msimamo wake, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, alimkashifu na kumtuhumu kusaliti viongozi wenzake wa Kikristo, kitendo kilichosababisha kukamatwa na kuhojiwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru