Thursday 16 April 2015

Wadaiwa sugu wa ardhiwafikishwa mahakamani


NA RACHEL KYALA
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imezifikisha mahakamani kampuni 11 ambazo ni wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi.
Miongoni  mwa kampuni hizo zinadaiwa ni S.H Amon, Highland Estate na Costix Limited  ambazo zinadaiwa sh. milioni 80.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba, Wilaya ya Ilala, Yose Mlyambina, alisema malalamiko dhidi ya kampuni na watu binafsi 120, yaliwasilishwa katika baraza hilo na Kamishna wa Ardhi, Dk. Moses Kusiluka.
Alifafanua kuwa S.H Amon, inadaiwa sh. milioni 38.2, Highland Estate sh. milioni 19.9 na Costix Limited sh. milioni 12.8.
Alisema Kamishna  wa Ardhi aliwasilisha madai hayo chini ya mfumo wa wadaiwa kutoruhusiwa kutoa utetezi isipokuwa kwa maombi maalumu ambapo mahakama hiyo itatoa siku 14 kwa watakaokuwa na hoja.
Mwenyekiti huyo alisema wananchi wanapaswa kutambua kuwa kulipa kodi ni wajibu wa msingi wa kila raia ili kuliongezea pato taifa ambapo Watanzania wengi wanapuuza suala hilo.
Mlyambina, alitaja madhara mengine ya baadhi ya watu na kampuni kutolipa kodi huku wengine wakilipa kuwa ni kuleta taswira ya mfumo wa kibaguzi na kuchochea wanaolipa kuacha kufanya hivyo.
Mhasibu Mkuu wa Wizara hiyo, Walter Lungu, alisema wizara ilichukua hatua ya kuwashitaki wadaiwa sugu baada ya kukagua hesabu zake na kugundua inapoteza kiasi kukubwa cha pato.
Alisema mbali na matakwa ya kisheria, hatua hiyo ni  utekelezaji wa amri ya Waziri William Lukuvi, aliyoitoa  kuanzia Januari  hadi Machi 30 kwa wadaiwa sugu kulipa, vinginevyo wangefikishwa mahakamani.
Kampuni zingine zilizofikishwa mahakamani ni Jessa Industries, St, Mary’s International Academy, St. Mary’s International Limited na Murzah Oil Mills,  Zake Construction Limited na Noor Investment Limited.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru