Thursday, 16 April 2015

Mtanzania aula AU


Na  Mwandishi Maalumu, New  York
BRIGEDIA Jenerali Sara Rwambali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ameteuliwa kuwa Mwakilishi Maalumu na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Afrika (AU), Sudan Kusini.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU,  Dk. Nkosanzana Zuma,  katika taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari alisema makazi ya Brigedia Jenerali Sara yatakuwa Juba.
Dk. Nkosanzana amemteua Josephine  Charlotte Kala kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kuwa Mwakilishi Maalumu na Mkuu wa Ofisi ya AU nchini Ivory Coast na makazi yake kuwa Abidjan.
Wengine walioteuliwa ni Madame Nyiramatama kutoka  Rwanda, anayekuwa Mkuu wa Ofisi ya AU nchini Chad  na  Dk. Arvin Boolel kutoka Mauritius anayekuwa Mwakilishi Maalumu wa AU  nchini Burundi.
Alisema uteuzi huo ni sehemu ya kuhakikisha uwepo  wake katika kila eneo na kuunga mkono juhudi zinazolenga kukuza amani na usalama barani Afrika.
Alisema mwaka huu AU imejikita katika uwezeshaji wa wanawake, hivyo anatumaini kwamba itanufaika na utaalamu na uzoefu mkubwa na uwezo wa kiuongozi kutoka kwa wateuliwa hao.
Mwenyekiti huyo pia alitoa wito kwa wadau wote kuwapa ushirikiano viongozi hao walioteuliwa ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa maslahi ya Afrika, huku akitoa shukrani kwa wawakilishi ambao wanamaliza muda wao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru