NA FURAHA OMARY
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewatangazia kiama
wahalifu, ambapo imeamua kuwasaka kwa kutumia helkopta, baada ya kupata taarifa
kwamba wamekimbilia mpakani mwa mkoa huo na wa Pwani.
“Tunaendelea na operesheni kali dhidi ya wahalifu, kwani tumepata taarifa kwamba kuna wahalifu wamekimbilia mpakani mwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani,” alisema Kamishna wa Kanda hiyo, Suleiman Kova.
Kamishna Kova aliyasema hayo mjini Dar es Salaam,
alipozungumza na Uhuru kuhusiana na hali ilivyokuwa wakati wa Sikukuu ya
Pasaka.
Alisema Sikukuu ya Pasaka imeisha salama kutokana na
kujiimarisha katika doria mbalimbali, zikiwemo za magari, pikipiki, Vikosi vya
Wanamaji, Mbwa na Farasi.
Pia alisema waliweka vituo vya muda katika fukwe za bahari na
doria ya ya helkopta ya polisi.
Aidha, Kamishna Kova alisema wameamua kutumia mashine za
ukaguzi kufanya ukaguzi wa kawaida kwa wananchi wanaotumia kivuko cha
Kigamboni.
Alisema lengo la ukaguzi huo ni kupambana na makosa
mbalimbali, yakiwemo ya ujambazi na ugaidi.
Akizungumzia operesheni ya wahalifu kwa kutumia helkopta,
Kamishna Kova alisema polisi imejipanga kupambana na wahalifu hao ambao kwa
sasa wana hali mbaya.
“Polisi Kanda ya Dar es Salaam, tunafanya kazi nzito kuhakikisha tunapambana na wahalifu, kwani tumeamua kutumia helkopta kuwasaka vichakani,” alisema.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru