Na Mwandishi Wetu
KIWANGO cha upatikanaji wa nishati ya umeme kinatarajiwa kupanda hadi asilimia 100 ifikapo mwaka 2030, umesema Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Meneja Utaalamu Elekezi wa REA, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, alisema hayo alipomwakilisha Mkurugenzi wa REA katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa wataalamu na wajasiriamali wa usambazaji vifaa vya umeme (nishati) itokanayo na mionzi ya jua.
Katika mafunzo hayo yanayomalizika leo katika Hoteli ya Kebis jijini Dar es Salaam, Mhandisi Nyamo-Hanga, alisema kiwango cha upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wananchi mijini na vijijini kimeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2007 hadi asilimia 36 mwaka 2015.
“Kiwango hiki kinatarajiwa kufikia asilimia 75 mwaka 2025 na asilimia 100 ifikapo mwaka 2030 ambao ni mwaka wa dira ya kimataifa ya ‘Nishati Endelevu kwa Wote.’
Meneja Mkuu wa Energy Plus, Bernadetha Daud, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwafanya wadau kujua namna bora zaidi ya kukisia uwezo wa mifumo na matumizi ya sola kwa watumiaji binafsi na taasisi.
“Unajua bado kuna uelewa mdogo kwa watu maana wengi hawajajua faida za matumizi ya sola… wengi wanadhani gharama za sola ni kubwa, lakini hawakumbuki kuwa umeme wa sola hauna malipo ya mwezi,” alisema.
Katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na kampuni ya Energy Plus ya Tanzania kwa kushirikiana na Africa Energy ya Marekani, Mhandisi Nyamo-Hanga, alisema teknolojia ya sola ina umuhimu wa kipekee kwa kuwa imewezesha watumishi wa umma kukubali kwa moyo kufanya kazi hata maeneo ya vijijini.
“Teknolojia ya sola ni jibu kubwa kwa matatizo ya umeme. Zamani kabla ya sola watumishi wengi walikuwa wakikataa kwenda kuhudumia vijijini maana wanajua hakuna hata umeme, lakini sasa wanakwenda bila shida,” amesema.
Mtendaji Mkuu wa Ageco Energy, Vincent Mughwai, alisema umeme wa sola una manufaa kwa kuwa unafika hata maeneo ya vijijini ambako bado ni ndoto kupata umeme toka gridi ya taifa.
Mshiriki mwingine ambaye ni Meneja Masoko na Mauzo wa Ensol Tanzania Limited, Samanchogu Kihore, alizitaja faida za matumizi ya sola kuwa ni pamoja na kutumika maeneo yote yakiwemo ya vijijini hata katika nyumba za nyasi, kutokuwa na gharama endelevu za kuzalisha na kutumia umeme kwa kuwa baada ya kuunda mfumo, hakuna gharama za malipo ya mwezi, mafuta wala matengenezo kwa kuwa haiharibiki kirahisi.
“Umeme wa sola hauhitaji nishati nyingine kama mafuta wala maji wakati wa kuuzalisha kwani unatumia jua ambalo halilipiwi na hauna kelele wakati wa kuzalisha wala kutumia, hivyo ni rafiki mkubwa wa mazingira,” alisisitiza.
Wednesday, 22 April 2015
REA: Upatikanaji wa umeme kuongezeka
08:37
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru