Tuesday, 7 April 2015

Watanzania Zimbabwe wataka rasimu ya katiba



Na Athanas Kazige, Harare
BAADHI ya Watanzania wanaoishi Zimbabwe, wameiomba serikali kupeleka Rasimu ya Katiba ili waisome na kuielewa vizuri.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi hapa, Apatae Fatacky, alisema hayo alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa habari hii, katika  klabu ya Watanzania iliyoko 6 Allan Willson.
Alisema wamekuwa wanafuatia rasimu hiyo kwa kusoma kupitia mitandao ya kijamii na kuomba kama kuna uwezekano wapelekewe vitabu angalau 10, katika ofisi ya ubalozi.

"Naiomba serikali ituletee angalau vitabu vitano au 10 vya rasimu ya katiba inayopendekezwa lengo ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata muda mwingi kuisoma na kuielewa vizuri," alisema.

Ofisa Balozi wa Tanzania, Zimbabwe, Issack Mwakililuma, alisema anawashukuru Watanzania wanaoishi nchini Zimbabwe kwa kufuatilia jambo hilo. 
Alisema wengi wao wamekuwa wanafuatilia mwenendo wa rasimu hiyo na wanasoma zaidi kwenye mitandao na vyombo vya habari.

"Kweli rasimu hazipo, lakini tupo kwenye mipango ya kuwasiliana na viongozi wetu kule nyumbani ili  watuletee,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru