Tuesday, 21 April 2015

Msaidizi wa Gwajima kortini


NA FURAHA OMARY
MSAIDIZI wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, George Mzava, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mzava (43), mfanyabiashara na mkazi wa Ilala, Dar es Salaam, alifikishwa  mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka ya kukutwa na bastola ya kiongozi huyo na risasi kinyume cha sheria.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, alimsomea Mzava mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Wilfred Dyansobera, baada ya mshitakiwa huyo kujisalimisha.
Mzava akisindikizwa na wakili wake, Peter Kibatala, alifika mahakamani hapo ili kusomewa mashitaka yanayomkabili katika kesi iliyofunguliwa Ijumaa iliyopita, ambayo washitakiwa wenzake watatu, akiwemo Gwajima, walisomewa mashitaka yao.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo, ambao walisomewa mashitaka yanayowakabili Ijumaa na kuachiwa kwa dhamana ni Askofu Msaidizi Yekonia Bihagaze na Mchungaji Geoffrey Milulu.
Katika kesi hiyo, washitakiwa wote wanne wanakabiliwa na mashitaka matatu.  Gwajima anakabiliwa na shitaka la kushindwa kuhifadhi silaha na risasi anazomiliki kihalali katika usalama huku wengine wakidaiwa kukutwa nazo kinyume cha sheria.
Akimsomea mashitaka yanayomkabili Mzava, Kweka alidai Machi 29, mwaka huu, katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni A, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa huyo na wenzake, Bihagaze na Milulu, walikutwa na bastola aina ya Bereta bila  kuwa na kibali au ruhusa kutoka katika mamlaka zinazohusika.
Katika shitaka la pili, Mzava na wenzake hao wanadaiwa siku hiyo wakiwa hospitalini hapo, walikutwa na risasi tatu za bastola na 17 za bunduki aina ya shotgun bila kuwa na kibali au ruhusa kutoka mamlaka zinazohusika.
Mshitakiwa huyo alikana mashitaka hayo, ambapo Wakili Kweka alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu Dyansobera alitoa masharti ya dhamana kwa kumtaka mshitakiwa kutia saini dhamana ya sh. milioni moja na kuwa na mdhamini mmoja mwaminifu atakayetia saini dhamana ya kiasi hicho.
Mshitakiwa alitimiza masharti hayo, hivyo aliachiwa kwa dhamana hadi Mei 4, mwaka huu, kesi itakapotajwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru