Thursday, 16 April 2015

Nyalandu atekeleza maagizo ya Kinana


NA MWANDISHI WETU, MBARALI
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amemaliza mgogoro wa ardhi uliokuwa ukifukuta kwa zaidi ya miaka saba kati ya wananchi wa vijijii 21 na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Nyalandu, ambaye yuko ziarani mjini hapa, jana aliwaeleza wananchi kuwa serikali haiwezi kuwaacha wananchi wake wakanyanyasika hivyo ni lazima ichukue hatua.
Uamuzi huo wa serikali wa kumaliza mgogoro huo, ni utekelezaji wa maagizo ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kuitaka serikali kuhakikisha inamaliza tatizo hilo.
Zaidi ya wananchi  1500 wa vijiji 21 wilayani Mbarali, walitakiwa kuhamishwa kutokana na madai ya kuingia kwenye mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, jambo ambalo limekuwa likipingwa kwa muda mrefu sasa.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini hapa jana, Nyalandu alisema serikali ya CCM ni sikivu na siku zote iko kwa maslahi ya wananchi wake.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi waliofika kusikiliza hatimaya maeneo yao, Nyalandu alisema msimamo wa serikali ni kuwalinda watu wake.
Alisema mgogoro huo umekuwa kero kubwa na kuwafanya wananchi kushindwa kuwa na uhakika wa maisha yao, hivyo serikali haiwezi kukaa kimya bila kuchukua hatua.
Alisema Kinana alitoa maelekezo kwa serikali na wananchi kukaa mezani na kutafuta njia za kumaliza tatizo hilo, ambapo kwa sasa limefikia mwisho.
“Serikali ya CCM ni sikivu na iko kwa ajiliya Watanzania. Hivi karibuni Mzee Kinana alipita hapa mkamweleza kero yenu na alifikisha malalamiko yenu serikali na niko hapa kwa ajili ya utekelezaji.
“Naomba niseme kuwa vijiji vinavyotakwa kuhama vitaendelea kuwepo na ninaagiza kufanyika kwa ukaguzi wa mpaka katika GN 28 ili kuhakikisha haki inatendeka katika suala hili.Huu mgogoro ni lazima ufike mwisho na uamuzi huu una baraka zote za Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,” alisema.

Alisema maeneo ambayo yana mgogoro mengi ndiyo kilimbilio na uchumi wa wananchi wa Mbarali kutokana na kuendesha shughuli za kilimo na makazi, hivyo serikali haiwezi kuchukua uamuzi ambao utakuwa na madhara kwa wananchi wake.

Kauli hiyo ya Nyalandu ilipokewa kwa furaha na wananchi waliofurika uwanjani hapo, ambao walisikika wakiimba nyimbo za kukipongeza CCM kwa kujali maslahi ya wananchi wake.
Kabla ya kuzungumza na wananchi hao, Nyalandu alikutana na uongozi wa CCM wilaya ya Mbarali pamoja na Kamati ya Siasa kuzungumzia mgogoro huo pamoja na kupata maoni.
Pia alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, ambapo alipewa taarifa kuhusiana na mgogoro huo na hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha mwafaka unapatikana.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbarali, Mathayo Mwangomo, alisema mgogoro huo umeleta mpasuko mkubwa na kusababisha wananchi kukosa imani na baadhi ya viongozi.
Alisema msimamo wa CCM ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi na kufanya shughuli za uzalishaji mali kwenye vijiji na maeneo wanayoishi, hivyo kutaka kuondolewa si sahihi.
Naye Mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi, alisema mgogoro huo umedumu kwa miaka mingi na kuwa ni lazima mwafaka ufikiwe ili kuleta amani na utulivu ambao umeanza kutoweka miongoni mwa wananchi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru