Wednesday 22 April 2015

Majambazi yavamia kanisani na kuiba


Na Clarence Chilumba, Ruangwa
WATU watano wamevamia na kuvunja madirisha ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Malolo na kuiba chombo kinachotumika kuhifadhia ekaristi takatifu (TABERNACULO).
Imeelezwa kuwa majambazi hayo yalidhani chombo hicho kimetengenezwa kwa dhahabu.
Tukio hilo lilitokea juzi, saa 8:30 usiku, baada ya majambazi hayo kuvunja madirisha ya kanisa hilo.
Kanisa hilo ni miongoni mwa makanisa makongwe na yenye historia kubwa hapa nchini, ambalo lilijengwa mwaka 1939.
Paroko wa kanisa hilo, Theophan Membe, alisema siku ya tukio alikuwa Lindi kuhudhuria misa takatifu ya mapadre wa jimbo la Lindi, iliyoongozwa na Askofu wa jimbo hilo Mhashamu Bruno Ngonyani.
Alisema baada ya tukio hilo alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kigango cha Malolo, Cleophas Nnonjela, na badaye walitoa taarifa polisi.
Membe alisema parokia ya Malolo ni miongoni mwa parokia zilizotoa wasomi wengi mkoani Lindi kutokana na historia yake.
Alisema kwa mujibu wa sheria za Roma za kanisa hilo, sehemu inayoibiwa Tarbenaculo, ukristo hufa mpaka wahusika walioiba kifaa hicho watakapokiri kuwa wameiba.
Membe alisema baada ya wahusika kukiri kama wameiba, askofu wa jimbo anaondoa dhambi ya mauti kutoka kwa waumini kwenda kwa wezi hao.
Alisema kutokana na kuibiwa kifaa hicho, waumini wa kigango hicho watakosa baadhi ya huduma ikiwemo ibada ya Jumapili, misa ya kila siku asubuhi, misa ya katekista na upigwaji wa kengele zinazoashiria saa kwa waumini.
Alisema katika kipindi hicho huduma za ubatizo, kipaimara, komunio takatifu, kitubio, misa za mazishi, mpako kwa wagonjwa, sherehe za ndoa na masuala yote ya msingi yanayohusu Kanisa Katoliki hayatakuwepo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru