Thursday 16 April 2015

Mengi afanya mazungumzo na Balozi wa Malawi


NA FURAHA OMARY
MWENYEKITI wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, amekutana na Balozi wa Malawi nchini, Hawa Ndilowe na kufanya mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali, yakiwemo ya kibiashara.
Dk. Mengi na Balozi Hawa walikutana jana, mjini Dar es Salaam, katika makao makuu ya kampuni za IPP.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Hawa alisema Malawi iko tayari kuingia ubia na Tanzania kwa ajili ya masuala ya kibiashara.
Pia, alimweleza Dk. Mengi, kwamba wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na sekta binafsi na kwamba nchi yake ipo tayari kuingia ubia na Tanzania.
Mbali na hayo, Balozi huyo alisema Malawi na Tanzania zinapaswa kujenga ushirikiano na kutumia fursa ya jukwaa la uwekezaji litakalofanyika Juni mwaka huu nchini Malawi.
Akizungumzia kuhusu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), Dk. Mengi alisema katika kukomesha mauaji hayo, hakuna budi kupambana na wauaji na wale wanaonunua viungo vya albino.
Kwa upande wake, Balozi Hawa alisema Malawi inaangalia kwa makini na imelipa uzito wa juu tatizo la mauaji ya albino.
Alisema Malawi inafanya kila jitihada kuona tatizo la mauaji ya albino linakwisha.
Balozi Hawa alisema hayo, baada ya Dk. Mengi kutaka kujua kutoka kwake, ushiriki wao katika mapambano na vitendo vya kinyama wanavyofanyiwa albino.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru