Tuesday, 14 April 2015

Wataka hotuba ya Rais ifanyiwe kazi


NA RABIA BAKARI
HOTUBA ya Rais Jakaya Kikwete aliyotoa katika mkutano wa viongozi wa dini inapaswa kutumika  kama dira na mwongozo hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Rais Kikwete alitoa hotuba hiyo hivi karibu na baadaye kuchapishwa katika vyombo vya habari. Alisisitiza umuhimu wa viongozi kusimamia amani na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu suala lililoibua hisia tofauti la Mahakama ya Kadhi.
Akizungumza na Uhuru jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Amani ya viongozi wa dini mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Musa Salum, alisema hotuba hiyo ni maridadi na isiachwe ipite.
“Naomba itumike kama dira ya kutuongoza, ni hotuba iliyoshiba na kujitosheleza katika kila kitu. ni mwongozo tosha,” alisisitiza Sheikh Salim.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema kamwe viongozi wa dini hawapaswi kuwa wachochezi au kuegemea upande wowote ule, bali kuwaongoza waumini kuepuka maasi na kumrudia Mungu.
Alisema cha kushangaza, baadhi yao wamegeuka wanasiasa na kuwashurutisha waumini wao nini cha kufanya na nini cha kuacha, kitu ambacho alisema si sahihi na kinaweza kuibua mtafaruku katika jamii.
Alisema lengo la kuundwa kwa kamati ya amani inayojumuisha viongozi wote wa dini ni kufanya mazungumzo na kusimamia misingi ya kiimani na kidini ili kuendeleza amani ya nchi ambayo ni tunu ya pekee kutoka kwa Mungu.
“Sisi viongozi wa dini tuna nguvu  kwa sababu tuna jamii kubwa ya watu. Tukianza kuporoshana hatutafika popote, hatutajenga bali tutabomoa,” alisema.
Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alisema anashangazwa na baadhi yao kuwataka waumini wajiandikishe kupiga kura na wapige kura ya hapana, sambamba na kutoichagua CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema hiyo ni kinyume na maadili, wawaache waumini wajichagulie kile wanachoona kinafaa na si kuingilia uhuru wa mtu wa kuamua.
Kikwete alisema Mahakama ya Kadhi serikali haitahusika na chochote bali kutoa mwongozo wa sheria, lakini kuendesha na kusimamia itafanywa na Waislamu wenyewe.
Jukwaa la Viongozi wa Dini ya Kikristo lilitoa tamko kuhusu mahakama hiyo na kuitaka serikali kutoendelea na msimamo wa kutaka iwepo nchini kwa kuwa ni kinyume cha utaratibu kwa kuwa serikali haina dini.
Nayo Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, ilisema viongozi wa dini hawapaswi kuipangia serikali nini cha kufanya na nini isifanye hususan kwenye mambo ya yanayohusu dini fulani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru