Na Antar Sangali, Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imezindua mradi wa kufunga vyombo vya mawasiliano ya meli na boti za uvuvi ili kuweza kuziona zikiwa baharini na kufuatiliwa kwa setalaiti kulinda usalama wa abiria pamoja na kupambana na vitendo vya uhalifu, usafirishaji dawa za kulevya, uharamia na ugaidi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alitoa msimamo huo wakati akihudhuria mafunzo ya mradi wa kuviona vyombo baharini vikitoa huduma au kufanya kazi za uvuvi na kuvifuatilia kupitia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano.
Balozi Seif alisema serikali imeanzisha mradi huo kwa vile Zanzibar ni kisiwa kinachojitegemea njia za usafiri wa baharini na anga na kwamba, kuna haja ya vyombo vya baharini kufungwa vyombo ili kukabiliana na uhalifu.
Alisema ili kukabiliana na uharamia na meli za uvuvi zinazovua kinyume cha sheria, usafirishaji dawa za kulevya na kulinda usalama wa watu, mradi huo umekuja wakati muafaka na utasaidia kuondoa vitendo ambavyo ni kinyume na utaratibu wa kisheria.
Makamu huyo alisema ili kufanikisha masuala hayo, umakini na utaalamu unahitajika katika kusajili vyombo hivyo ili wavuvi wadogo wasishindwe kulipia gharama za huduma baada ya kila boti kutakiwa kufungwa vifaa hivyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Maalim, alisema teknolojia itakayotumika chini ya mradi huo ni mpya ambayo itasaidia kubaini vyombo vilivyopata usajili moja kwa moja vinapokuwa baharini huku watendaji wakibaki ofisini.
Maalim alisema kila mkoa utakuwa na kituo cha kupokea mawasiliano na ZMA itaandaa kanuni maalumu kuhakikisha vyombo vyote vya usafiri na uvuvi vinasajiliwa kwa mujibu wa sheria.
Naye Mtendaji Mkuu wa SRT Technology kutoka Uingereza, Simon Tucker, alisema teknolojia hiyo ya mawasiliano imeleta mafanikio kwa nchi zilizokuwa zikikabiliwa na tatizo la biashara haramu za magendo, uharamia na ugaidi.
Tucker alisema teknolojia hiyo imetumiwa na nchi mbalimbali za visiwa ikiwemo Madagascar, Saud Arabia, Vietnam ambapo imesaidia kuondoa matatizo ya uvuvi haramu na kukabiliana na matukio ya utekaji meli kwa muda muafaka.
Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya sh. bilioni 60 na vifaa vitafungwa huku kila chombo kikitakiwa kugharamia ufungaji wa vyombo hivyo.
Saturday, 18 April 2015
Meli Zanzibar kufuatiliwa kwa setilaiti
09:29
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru