NA CHRISTOPHER LISSA
HATIMAYE serikali imeumaliza rasmi mgogoro wa ardhi uliodumu kwa kipindi kirefu baina ya Wizara ya Maliasiali na Utalii na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, unaohusisha eneo Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Aidha serikali imeiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo , kukaa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na wadau, kurejea mipaka ya zamani ya eneo hilo, ili kuepusha mgongano usio na tija.
Mgogoro huo uliibuka mwaka mwaka 2005, baada ya serikali kuipandisha hadhi mbuga ya wanyama pori ya Saadani kuwa Hifadhi ya Taifa na kumpa mwekezaji.
Alisema eneo hilo lilitolewa kwa mtu aliyefahamika kwa jina la Lazaba, kutoka Zanzibar, kwa ajili ya shughuli za kunenepeshea mifugo, ambapo wananchi walilalamikia kuwa mipaka mipya ya hifadhi hiyo iliingia katika eneo lao, hali iliyoibua mgogoro mkubwa baina yao, TANAPA na mwekezaji.
Tamko hilo la kumaliza mgogoro huo limetolewa hivi karibuni na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye alitembelea eneo la mgogoro pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Saadani, akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Adelhelm Meru, pamoja na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Bagamoyo na TANAPA.
Nyalandu alisema kuwa ameamua kumaliza rasmi mgogoro huo, baada ya kuridhishwa na taarifa aliyopewa na Katibu Mkuu wake Dk. Meru, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Abdulkadir Lamiya na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Shukuru Mbato.
Alisema kuwa mgogoro huo hauna tija kwa maendeleo ya taifa, kwani dhima ya wizara yake ni kuona maeneo yote tengefu, zikiwemo mbuga za wanyama, vivutio mbalimbali, mapori ya akiba na hifadhi za taifa yanakuwa ni maeneo rafiki kwa watu wanaoishi jirani.
“ Serikali italinda kwa nguvu zote maeneo hayo ili kutunza raslimali pamoja na mipaka iliyowekwa. Ni marufu kuachia maeneo hayo muhimu.
Itakuwa siyo busara kuendeleza migogoro isiyo na tija kama huu wa Bagamoyo, ambao haukuwa na ulazima wa kuwepo.
Hakuna haja ya wananchi wanaoishi karibu na hifadhi zetu kuishi kwa mashaka na kujenga uhasama na wawekezaji au walinzi wetu wa maeneo haya,” alisema Nyalandu.
Aliongeza: “Nikiwa waziri mwenye dhamana, ninatamka kuwa mgogoro huu umemalizwa rasmi na ninaagiza TANAPA na Halamshauri ya Wilaya ya Bagamoyo kurejea upya mipaka iliyokuwepo awali kwa mujibu wa sheria. Pia ninaagiza GN namba 281 ya mwaka 2005, ifanyiwe marekebisho haraka na kuiwasilisha kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ili kuhakikisha kuwa mgogoro huu unamalizika kabisa.”
Nyalandu aliagiza kuwa eneo la mgogoro la Lazaba, wananchi wapange matumizi endelevu kwa kuzingatia zaidi kwamba eneo hilo liko karibu na Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Awali, Katibu Mkuu alimweleza Nyalandu kuwa mgogoro wa eneo la Lazaba ulidumu kwa muda mrefu na kusababisha shughuli za maendeleo katika eneo hilo kusimama.
“Wawekezaji wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo katika eneo hili. Pia wananchi wanaogopa kuingia katika eneo la hilo na kuyaendeleza maeneo yao.
Akieleza historia fupi ya mgogoro huo, Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mbato, alisema kuwa mwaka 1976, eneo hilo lilitolewa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kwaajili ya kutumika kama eneo la kunenepeshea mifugo.
“Hata hivyo, wakati serikali ikiipandisha hadhi mbuga ya wanyama pori ya Saadani kuwa Hifadhi ya Taifa, wakati wanapima mipaka, ilionekana sehemu hiyo ya mgogoro imeingia kwenye eneo la wananchi, hivyo kuibua mgogoro mkubwa baina ya TANAPA na wananchi wa eneo hilo, pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.
Tuesday, 14 April 2015
Serikali yamaliza mgogoro Hifadhi ya Saadani
08:23
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru