NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imedhamiria kuwarudisha nchini Watanzania waishio Yemeni, kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Ali Ahmed Saleh.
Alisema ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa Watanzania hao ambao wengi ni wanafunzi, wanarudi nchini wakiwa salama.
Membe alisema awamu ya kwanza ya kuwarudisha ilifanyika hivi karibuni chini ya uratibu wa Ofisi za Ubalozi wa Tanzania ulioko mjini Mascut, Oman.
Alisema katika awamu hiyo Watanzania 25, walirudishwa na kwamba juhudi za kuwarudisha wengine zinaendelea.
“Nimeruhusu matumizi ya fedha ya dharura ili kuhakikisha ndugu zetu walioko kwenye hatari na machafuko yanayoendelea Yemen wanarejeshwa salama,” alisema.
Alisema Watanzania hao wengi wao wamefika katika miji ya Sarfat na Al-Mazyouna iliyoko katika mpaka wa Oman na Yemen.
Membe alisema raia hao walituma maombi ya dharura kwenye ofisi za ubalozi, kuelezea mazingira ya hatari yanayowakabili operesheni ya kuhakiki, kuadnikisha na kuwarudisha lilianza mara moja.
Alisema awamu ya pili ya kuwahakiki itaanza hivi karibuni, ambapo Watanzania 64 wataruhusiwa kuingia Oman na kurejeshwa Tanzania.
Membe yuko Oman kwa ziara ya siku moja ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru