Wednesday, 22 April 2015

TASAF yafafanua


NA Lisa Said, Tanga
MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleleo ya Jamii (TASAF), Ladislaus Mwamanga, amesema kuwa mfuko huo kutoa fedha kwa ajili ya kuziwezesha kaya masikini sio kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali ni mipango ya serikali kuleta unafuu wa kipato kwa wananchi wake.
Aliyasema hayo hivi karibuni katika kikao cha kazi kilichowashirikisha wadau wa mfuko huo kutoka Halmashauri za Mkoa wa Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Zanzibar wakiwemo waratibu wa TASAF wilaya na mkoa, waandishi, maofisa wafuatiliaji  na wahasibu kwenye halmashauri.
Pia, Mwamanga alisema kuwa muungano waliouweka kati ya watumishi wa halmashauri na waandishi hao sio ‘ndoa ya mkeka’ bali ni endelevu lengo likiwa kuona wanashirikiana na kuufanya mfuko huo ulete tija kwa wananchi.
“Mpango huu unaofanywa na TASAF kugawa fedha kwa kaya masikini si wa CCM kama watu wanavyoghani, mpango huu ni wa serikali katika kuzikwamua kaya masikini kiuchumi na kuleta maisha bora kwa Watanzania wote,” alisema.
“Ili kuonyesha kinachofanywa ni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, mpango huu umewashirikisha waandishi wa habari. Muungano huu haujawahi kutokea, na waandishi msije mkadhani muungano huu kati yenu na sisi ni ndoa ya mkeka, bali ni jambo endelevu,” alisema Mwamanga.
Mwamanga alisema kwa kuwashirikisha waandishi kwa kina kwenye Mpango wa TASAF III ni kuwasaidia kuweza kuandika habari zilizo sahihi na wasikubali kupotoshwa na baadhi ya watu, ambao hawajui nia yao ni nini.
Alisema TASAF imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na ndiyo mradi mkubwa barani Afrika ambao umewezesha kuwafikia wananchi wengi, huku ukionekana jinsi unavyofanya kazi kuanzia matumizi ya fedha na uratibu wake, hivyo waandishi na wananchi ni vyema wauunge mkono.
Mratibu  wa TASAF wilaya  ya Lushoto, Beatrice Shemdoe, alisema kuwa  wilaya yao imejipanga kunufaisha kaya za watu masikani 10,779 ikiwa  ni  kutoka  katika vijiji 146 kwa kuziwezesha kupata uhakika wa chakula, gharama za matibabu  na elimu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru