Thursday 16 April 2015

IGP Mangu awapa neno Waislamu


NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu, ameungana na viongozi wa dini ya Kiislamu kukemea vitendo vya uhalifu.
Ili kudhibiti vitendo hivyo, amezitaka familia kutoa malezi bora kwa watoto  ili kuondokana na wimbi la watu wanaojiingiza makundi yanayofanya mambo hayo.


IGP Mangu alisema hayo jana katika  mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa Kiislamu katika kuimarisha usalama nchini yenye kauli mbiu isemayo ‘Amani na usalama ndio maisha yetu’.
Mafunzo hayo yaliratibiwa na Taasisi ya Mwinyi Baraka na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu nchini.
IGP Mangu alisema viongozi wa dini wana dhamana kubwa katika kuhakikisha vitendo vya uhalifu vinadhibitiwa kwa kuwaelimisha waumini wao na jamii kwa ujumla juu ya madhara ya uhalifu na kuwapa mafundisho yatakayojenga na kuimarisha ulinzi na usalama. 
Naye Mwakilishi wa Sheikh Mkuu wa Tanzania, ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Ulamaa la BAKWATA, Sheikh Abubakar Zuber, alisema kuna haja ya kuziba nyufa za uvunjifu wa amani ambazo zimeanza kujitokeza.
Alisema ni muhimu kuziba nyufa hizo kwa kuanzia kwenye misikiti, familia na hatimaye katika jamii zinazowazunguka ili kuhakikisha nchi inaendelea kubaki salama.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wanazuoni wa Kiislamu, Sheikh Khamis Mataka, alisema uhalifu unaweza kujitokeza sehemu yoyote hata ndani ya msikiti, hivyo ni jukumu la viongozi wa misikiti kuwafichua wahalifu.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwinyi Baraka, Sheikh Issa Othman, alisema wataendelea kutoa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo viongozi wa dini kuwaelimisha waumini wao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru