Sunday 2 March 2014

CCM yakerwa vijana kutumika kuvunja amani



Na Suleiman Jongo
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kinasikitishwa na baadhi ya vyama vya siasa ambavyo vimejenga utamaduni wa kuwatumia vijana  kufanya vurugu na maandamano yasiyo na tija zaidi ya kuweka mazingira ya umwagaji damu.
Hayo yalisema jana na Mwenyekiti wa  CCM, Mkoa wa Iringa Joyce Nsambatavangu, wakati akimdani mgombea wa CCM katika jimbo la Kalenga mkoani hapa, Godfrey Mgimwa.
Alisema ni jambo la ajabu wakati serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuandaa vijana, lakini wanapofikia umri wa miaka 15 na kuendelea, vinatokea vyama vya siasa vinatumia nafasi ya uwepo wao kufanya vurugu.
"Ni jambo baya kuona  vijana ambao wamegharamiwa kwa fedha nyingi wanatumika kuvuruga amani ya nchi hii na katika hilo Chama na serikali havitakubali yafanyike," alisema.
Alisema ni vyema Watanzania watambue baadhi ya vyama vya upinzani kuwa havina nia njema na taifa kwa kuwa viko tayari kufanya kila aina ya hila kuhakikisha amani ya nchi inatoweka na wanaotumika kufanya hilo ni baadhi ya vijana ambao wanatumiwa kwa maslahi ya vyama hivyo.
Alisisitiza kuwa CCM haiko  tayari kuona vijana ambao wamekuzwa kwa gharama kubwa wanaingizwa kwenye makundi ya vurugu na fujo na muda mwingi ukitumika katika maandamano yasiyo na tija.
"Inasikitisha baadhi ya wanasiasa ambapo wanatumia kila mbinu kuhamasisha vijana kufanya vurugu na matukio mengine yanayoashiria umwagaji damu nchini,"alisisitiza
Pia alisema wananchi washirikiane na CCM katika kuleta maendeleo kwa kutumia makundi yote nchini na huku akitumia nafasi hiyo kuwataka wachukie vyama vinavyohamasisha vurugu na fujo kwa kutumia vijana.
Pamoja na hayo, aliwataka wananchi kutofanya makosa katika siku ya uchaguzi ambayo ni Machi 16, mwaka huu, kwa kumpa kura Mgimwa ili aweze kuleta maendeleo katika jimbo hilo na kwamba hakuna sababu ya kuchagua upinzani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru