Tuesday 25 March 2014

Mkurugenzi Bodi ya Utalii ang’olewa


NA KHADIJA MUSSA
MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dk. Aloyce Nzuki, ameng’olewa katika wadhifa huo, kutokana na utendaji usioridhisha.

Add caption

Uamuzi wa kung’olewa Dk. Nzuki ulifikiwa jana baada ya awali Bodi ya Wakurugenzi ya TTB kuwasilisha mapendekezo wizarani kutaka aondolewe.Hata hivyo, kabla ya kufikiwa uamuzi huo jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alikutana na Bodi ya TTB kuzungumzia kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa kwake.
Kikao cha pamoja kilihudhuriwa na wajumbe wa Bodi ya TTB, akiwemo Mwenyekiti, Charles Sanga, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamoud Mgimwa, Katibu Mkuu Maimuna Tarishi na Naibu Katibu Mkuu, Selestine Gesimba.
Kutokana na hoja zilizowasilishwa na bodi, Nyalandu aliridhia kung’olewa kwa Dk. Nzuki, ambaye atapangiwa kazi nyingine na nafasi yake kukaimiwa na Devota Mdachi.
Devota ni Mkurugenzi wa Masoko wa TTB. Nyalandu ameagiza mchakato wa kumpata mtendaji mwingine wa taasisi hiyo uanze mara moja na uwe umekamilika ndani ya siku 21.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao kilichofanyika wizarani, Sanga alisema mapendekezo ya kutaka Dk. Nzuki kuondolewa ni ya muda mrefu.
Alisema Dk. Nzuki ameshindwa kufanya kazi inayotakiwa, hivyo bodi ilipendekeza kwa waziri mwenye dhamana kuingilia kati kuiwezesha TTB kusonga mbele kwa ufanisi.
Sanga alisema katika utendaji kazi suala la uzalendo na utaifa ni muhimu likazingatiwa na kwamba, bodi itahakikisha inafanya kazi kwa ufanisi.
Nyalandu alisema ameridhia mapendekezo hayo baada ya kupokea barua iliyotiwa saini na wajumbe wa bodi ya TTB, ikimshauri amuondoe Dk. Nzuki.
Alisema azma ya serikali ni kuhakikisha sekta ya utalii inakua kwa kasi na kwamba, kupumzishwa kwa Dk. Nzuki hakuna maana kuwa amekosea, bali ni utaratibu wa kawaida serikalini.
Nyalandu aliagiza bodi kuitangaza nafasi hiyo ili Watanzania wa ndani na nje wenye sifa za kuomba wafanye hivyo ndani ya siku 21 kuanzia leo.
Aliitaka bodi kuhakikisha kasi ya kuutangaza utalii na vivutio vyake inaongezeka maradufu na asingependa kusikia majibu ya kushindwa na nchi jirani, ikiwemo Kenya

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru