Sunday 2 March 2014

Mwigulu ataka Mbowe, Dk. Slaa washitakiwe

Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba

  • Awashangaa polisi kuwaacha wakitanua
NA SULEIMAN JONGO, IRINGA
MWENYEKITI wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake Dk. Willibrod Slaa, wanatakiwa kushitakiwa kwa matukio ya umwagaji damu nchini, imeelezwa.
Pia, vyombo vya dola vimelaumiwa kwa kukaa kimya bila kuwachukulia hatua zakisheria licha ya kushiriki katika matukio yaliyopoteza maisha ya Watanzania.
Hayo yameelezwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, ambapo alisema licha ya viongozi hao kushiriki kwenye matukio mengi ya vurugu na umwagaji damu, lakini bado wako nje wakiendelea kutanua.
Alisema iwapo uchunguzi wa kina utafanyika ni dhahiri Mbowe na Dk. Slaa hawatasalimika na kwamba, ushahidi wa matukio upo hadharani.
Mwigulu alikuwa akizungumza katika Kijiji cha Magubike, kata ya Nzihi wilayani Iringa wakati akimnadi mgombea wa CCM Godfrey Mgimwa, kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la Kalenga utakaofanyika Machi 16, mwaka huu.
Alisema Dk. Slaa na Mbowe wanahusika na vifo vya watu vilivyotokea kwenye vurugu mbalimbali katika mikutano ya hadhara ya chama hicho.
"Hawa watu wameshiriki kwenye matukio mengi ya vurugu na yanafahamika, lakini hawajachukuliwa hatua. Uchunguzi wa kina ufanyike kwani wote hawa wanahusika moja kwa moja.
"Mikono yao imejaa damu za watu waliopoteza maisha Morogoro, Singida Arusha na maeneo mingine ya nchi yetu," alisema Mwigulu.
Alisema vurugu zote ambazo zimefanywa na CHADEMA lengo ni kufanikisha mikakati yao kisiasa, jambo ambalo wananchi wa Kalenga wanapaswa kuliepuka na kuwa makini nao.
Alisema kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka huu tayari vifo vya watu zaidi ya nane vimetokea katika mikutano ya Chadema na kwamba, hali hiyo inapaswa kuonywa vikali na wapenda amani wote.
Pia, alisema viongozi hao wamekuwa wakifadhili matukio ya vurugu kisha kijitokeza kusaidia familia za waathirika.
Akitoa mfano kwa Mussa Tesha, aliyemwagiwa tindikali mkoani Tabora wakati wa uchaguzi mdogo jimbo la Igunga na Alphonce John, aliyetobolewa macho wilayani Kahama, Mwigulu alisema viongozi hao walihusika na mipango hiyo.
‘’Historia inaonyesha kuwa hawa watu wakiwa kwenye mikutano mauaji ni lazima. Tumechoka ni unyama huu sasa tunataka hatua kali zichukuliwe ili kulinda maisha ya watanzania,’’ alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Kalenga kukataa viongozi hao kwani, mara zote wamekuwa wakitumia ubabe na vitisho kutaka kupigiwa kura.
"Ni vizuri wakamchagua kijana ambaye anaweza kufanya kazi katika mazingira ya amani na utulivu ili kuzitatua changamoto zilizopo," alisema Mwigulu.
Pamoja na hayo, alitumia nafasi hiyo kuweka wazi Watanzania wanatakiwa makini na vyama vya siasa vyenye lengo la kuvuruga amani kuwa, CHADEMA hunufaika na vurugu hizo kupitia wafadhili wao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru