Tuesday 25 March 2014

Watendaji wabovu waadhibiwe -Kinana


NA SULEIMAN JONGO
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ametaka wana-CCM kuwa wakali dhidi ya watendaji wabovu na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama.

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akishuka kutoka kwenye tanki la mradi wa maji katika eneo la Tabata Kimanga, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wakati wa ziara yake, wilayani Ilala, Dar es Salaam, jana. Tanki hilo lenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo 200,000 za maji litakapokamilika litahudumia wakazi wa maeneo wa Tabata Kisiwani na Tabata Kimanga. Picha zaidi.uk.18. (Na Bashir Nkoromo).

Ameagiza kusimamiwa miradi ya Chama na kutokubali wachache wanufaike zaidi kuliko CCM.
Kinana alisema hayo jana wilayani Ilala, Dar es Salaam, alipozungumza na wana-CCM kwa nyakati tofauti akiwa ziarani.
Alisema baadhi ya watendaji wa CCM na serikali kwa makusudi wamekuwa wakikwamisha maendeleo, ambayo ni kiunganishi kati ya Chama na wananchi wanaoendelea kukiweka madarakani.
Kinana alisema huu si wakati wa kuendelea kuwatazama watendaji wa aina hiyo, ambao wanadumaza maendeleo bali wachukuliwe hatua stahili na kwa wakati muafaka.
Katibu mkuu alisema ni vyema kila kiongozi akahakikisha anatekeleza wajibu wake kikamilifu ili kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM, iliyoahidi kutatua changamoto mbalimbali, zikiwemo za miundombinu, nishati, maji na afya.
Alitaka kila kiongozi, wakiwemo wa serikali na waliowekwa madarakani na wananchi, akajipima kabla ya kupimwa na wapiga kura au mamlaka yake ya uteuzi.
“Hatuko tayari kumuacha yeyote tunayeona anatupeleka kusikotakiwa au kwenda kwa kasi isiyoendana na malengo yetu. Wana-CCM kokote mliko hakikisheni mnawabana watendaji wabovu ili wafanye kile tulichoahidi kwa wananchi,” alisema.
Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya siku nne mkoani Dar es Salaam, alisema huu si wakati wa kuendekeza umangimeza na kutowajibika kwa kuwa Watanzania wanataka kuona maendeleo na utekelezaji ahadi.
“Watanzania wamechoshwa na maneno na ahadi zisizotekelezeka, wanataka vitendo. Tutawabana viongozi wanaoendekeza umangimeza badala ya kusimamia maendeleo na kuwatumikia wananchi,” alisema.
Alisema baadhi ya watendaji wamekuwa wakijisahau kwa kukaa ofisini, kwa kuwa wana uhakika wa kupokea mshahara, huku wananchi waliowapa uongozi wakitaabika na kuvuja jasho kutafuta maendeleo.
“Ikiwa tutatekeleza mkataba  tulioingia na wananchi katika uchaguzi mkuu mwaka 2010, ni wazi Watanzania watatuamini tena kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani. Tukifanya tofauti na tuliyoahidi katika Ilani, tutambue watatushangaa na kutubeza,” alisema.
Kinana alisema CCM haiko tayari kuona kikundi cha watu kikiandaa mikataba mibovu, ambayo haikinufaishi Chama.
“Viongozi wa CCM wa ngazi zote simamieni miradi ya maendeleo kikamilifu. Sehemu iliyo na matatizo ya mikataba undeni tume na kufanya uchunguzi. Haiwezekani watu wachache kuingia mikataba mibovu isiyokinufaisha Chama,” alisema.
Alisema hayo baada ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Asaa Simba, kueleza Chama wilayani humo kinakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ya mikataba mibovu ya miradi.
Simba alimuomba Kinana kusaidia harakati za kuwapata wanasheria wa CCM kutoka makao makuu ili kusimamia urekebishaji wa mikataba hiyo.
“Moja ya changamoto tulizozikuta wakati tukiingia madarakani ni mikataba isiyoridhisha. Mfano hapa tulipo (makao makuu ya CCM Wilaya ya Ilala) fremu zinakodishwa kwa sh. 250,000 kwa mwezi kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na maeneo mengine. Mkataba huo ni wa miaka 35,” alisema.
Kinana alitembelea miradi ya maji na shule katika kata za Buguruni, Tabata Kisiwani na Gerezani. Leo atakuwa wilayani Temeke.
Wakati huo huo, CCM Wilaya ya Ilala imemuomba Kinana, kuingilia kati sakata la madereva wa bodaboda kuzuiwa kuingia katikati ya jiji.
“Ndugu Katibu Mkuu tunakuomba uingilie kati suala la madereva wa pikipiki kuingia katikati ya jiji kwa kuwa ni tatizo lililowagusa wengi, wakiwemo madereva na abiria,” alisema Simba.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru