Wednesday 5 March 2014

Mbinu kuhujumu bunge zafichuka


  • Wanasiasa, wanaharakati wahusishwa
  • Wabunge wacharuka, wampongeza Pengo

Na Theodos Mgomba, Dodoma

MCHEZO mchafu unaofanywa na baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa na wanaharakati kutaka kuvuruka Bunge Maalumu la Katiba, umebainika.
Habari za kuaminika ambazo Uhuru ilizipata jana, zinadai kuwa mikakati hiyo inaratibiwa kwakaribu na baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani, ambao kwa namna moja ama nyingine, wana malengo binafsi.
Kubainika kwa mikakati hiyo kumekuja ikiwa ni siku moja tu tangu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kukanusha kuwa Kanisa hilo limetoa msimamo wa kupendekeza serikali tatu.
Mwadhama Pengo alisema juzi mjini Dar es Salaam kuwa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kuwa msimamo wa kanisa ni serikali mbili sio sahihi na hawaitambui.
Pia, alisema angependa kuona mfumo wa serikali mbili ukiendelea kwani kuwa na serikali tatu ni mzigo kwa Watanzania na kwamba, iwapo kuna dosari zirekebishwe.
Alisema waraka huo ulitolewa na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), na wala si msimamo wa Kanisa Katoliki.
Wakizungumza na Uhuru mjini hapa jana, baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walisema dalili zote za kuvurugwa kwa bunge hilo zimeonekana.
Pia, walisema wana taarifa za ndani kuhusu baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kujaribu kuwashawishi wajumbe kugomea ama kuanzisha mjadala bungeni hata kwenye mambo yasiyo na msingi.
Wajumbe hao wakiongozwa na Mussa Azzan Zungu (Ilala-CCM), walisema wamenasa mipango mbalimbali inayoratibiwa na baadhi ya viongozi hao, ambao hawana nia njema na taifa.
Zungu alisema pamoja na kuandaa mikakati hiyo ambayo tayari mingine imeanza kukataliwa ikiwemo waraka waliouita ‘feki’ uliotolewa na Kanisa Katoliki wa kutaka kulazimisha serikali tatu.
“Kuna mchezo mchafu unaendelea kwa sasa lengo likiwa kukwamisha bunge hili kutokana na matakwa ya wachache kutopewa kipaumbele. 
“Tumenasa mbinu hizo na tutazifikisha kwenye vyombo husika na kisha tutashitaki kwa wananchi…watu wanataka kupata umaarufu kwa kuwaumiza watanzania wenzetu, kwa hili, hatutakubali.
“Sisi kama wabunge wa CCM, tunampongeza Kadinali Pengo kwa kuwa muwazi na kuukana ule waraka ambao ulianza kuleta sintofahamu. Wengine wameanza kutumia nyumba za ibada kutunga uwongo ili kuharibu hii kazi,’’ alisema.
Alisema kuna vipeperushi na nyaraka zingine zimeanza kusambazwa zikidai kuwa CCM hawataki katiba mpya, jambo ambalo halina ukweli na limezushwa ili kuwaghilibu watanzania.
“Serikali ni ya CCM na ndio iliyoridhia kuwa Katiba yetu ya sasa iboreshwe ili kwenda na wakati, halikuwa kwenye Ilani, lakini JK (Rais Jakaya Kikwete) kwa mapenzi na nchi yake, akasema hili lifanyike, sasa mtu anasimama eti CCM inapinga, huyu atakuwa mzima kweli,’’ alihoji Zungu.
Naye Haji Omari Kheir, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Idara Maalumu) wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alisema mipango inayoratibiwa na wanasiasa hao ni pamoja na ya kupandikiza chuki za kuvunja Muungano.
Alisema wapo wanasiasa ambao wamejipanga kuhakikisha Muungano unavunjika kutokana na uchu na tamaa ya madaraka.
“Tutasimama imara kupinga aina yoyote ya udhalimu huu, wakae wakifahamu kuwa Muungano badala ya kuvunjika sasa utakuwa imara zaidi,” alisema. 
Pia, alimpongeza Kardinali Pengo na kusema wao kama wawakilishi wa wananchi, watasimama imara kupinga usultani au ubabe unaotaka kutumika ili kuharibu bunge hilo kwa lengo la kukwamisha mchakato mzima wa upatikanaji wa katiba mpya.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru