Thursday 6 March 2014

Mwampamba: CHADEMA wasiwarubuni


Na Mwandishi wetu.
MKUU wa Kitengo cha Mawasiliano cha Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mtela Mwampamba, amesema mgombea wa chama hicho katika uchaguzi wa jimbo la Kalenga, Godfrey Mgimwa ni raia wa Tanzania.
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akimnadi mgombea huyo katika Kijiji cha Lupembelwasenga.
Alisema CHADEMA baada ya kukosa ajenda katika kampeni za uchaguzi huo unaotarajia kufanyika Machi 16, mwaka huu, walianza  kumzushia Mgimwa kuwa si raia wa Tanzania.

“Achaneni na uzushi huo wa CHADEMA, hawana jipya, wamezidiwa nguvu na CCM sasa wanatapatapa.
“Mgimwa ni raia na mzaliwa wa Kalenga, ogopeni uzushi huu,” alisema Mwampamba.
Alisema, Mgimwa baada ya kumaliza elimu yake ya msingi mkoani Iringa, alikwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na masomo ya sekondari na baada ya hapo akaenda Uingereza kwa ajili ya masomo.
Alisema kitendo cha Mgimwa kwenda masomoni nje ya nchi ndicho kinachowafanya CHADEMA wadai kuwa si raia wa Tanzania.
“Puuzeni uongo huu, familia na ukoo wa marehemu Dk. William Mgimwa unafahamika vizuri kwa kila mmoja,” alisema.
“Maana kama Godfrey alikwenda Uingereza kusoma, CHADEMA wanasema si Mtanzania, maana yake hata marehemu Dk. Mgimwa alipowenda kutibiwa Afrika Kusini, basi wangesema ni Mwafrika Kusini,” alisema.
Hivyo, Mwampamba aliifananisha CHADEMA na mtoto ambaye hajui uhusiano wa baba na mama kwa maana  ya maendeleo yaliyopo katika jimbo hilo msingi wake ni CCM na Dk.Mgimwa.
“Barabara, zahanati, maji na ujenzi wa shule za kata, msingi wake ni Serikali ya CCM na utekelezaji ulikuwa unasimamiwa na Dk. Mgimwa.
Hivyo, tunachofanya sasa ni kumpata mbunge atakae endeleza,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru