Wednesday 5 March 2014

Jaji Salome: Viongozi acheni kuvujisha siri


  • Aonya ubinafsi wa watumishi utavuruga amani

Na Mohammed Issa

VIONGOZI na watendaji wa serikali wameonywa kuacha tabia ya kutoa siri za serikali na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Pia, wameonywa kuacha ubinafsi kwa kuwa uvunjifu wa maadili na amani nchini kwa kiasi kikubwa umesababishwa na vitendo hivyo.
Onyo hilo lilitolewa jana na Kamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda, alipofungua mafunzo ya maadili kwa viongozi wa taasisi za Wizara ya Maji.
Mafunzo hayo yanahudhuriwa na watumishi kutoka taasisi zilizochini ya wizara hiyo ikiwemo DAWASA, EWURA, SUMATRA, Wakala wa Visima na Mabwawa na PPRA.
Alisema katika siku za hivi karibuni baadhi ya viongozi wa umma wameendelea kukiuka maadili ya utumishi kwa kutoa siri za serikali kinyume cha sheria.
Jaji Salome, alisema vitendo vya rushwa vimekithiri kila sehemu na kwamba, vingine vinafanywa na viongozi wa umma.
“Kuna rushwa za kuwekeza utaona mtu anataka mchango wa harusi wa sh. milioni 12 ambazo hata baadhi ya viongozi wanajihusisha nazo. Sheria ya maadili inaruhusu kupokea zawadi, lakini sio rushwa,” alisema.
Jaji Salome alisema kiongozi wa umma kumiliki mali sio kosa, lakini mali hizo awe anazimiliki kihalali.
Alisema wakati umefika sasa kwa viongozi wa umma kuacha kutumia mali za serikali yakiwemo magari kinyume cha sheria.
Jaji huyo mstaafu, alisema bado kuna matatizo ya kimaadili katika utumishi wa umma na jamii na kwamba utoaji huduma hauridhishi, kuna matumizi mabaya ya madaraka, wizi na ubadhirifu wa mali za umma na kujilimbikizia mali zisizo halali.
Jaji Salome alisema lengo la mafunzo hayo ni kuinua maadili katika utumishi wa umma na ni muendelezo wa mkakati wa kukuza maadili nchini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi, alisema mmomonyoko wa maadili umejipenyeza kila sehemu.
Aliwataka viongozi wa umma kufanyakazi kwa bidii na uadilifu na aliiomba sekretarieti kutoa maoni kuhusu mmomonyoko wa maadili nchini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru