Sunday 2 March 2014

CCM yashitukia mchezo mchafu



  • Wawakilishi Z’bar wasisitiza ni serikali mbili
  • Waponda maoni ya BLW kwenda kwa Warioba
  • Sheni apigilia msumari, waraka feki wakwama
Na waandishi wetu
WAJUMBE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Baraza la Wawakilishi, wamedai wao si sehemu ya maoni yaliyowasilishwa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pia, wameponda mchezo mchafu wa baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar kusambaza waraka kudai msimamo wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW) unaunga mkono mfumo wa serikali tatu kuwa, hawautambui na kuwa umetengenezwa na wajanja wachache kwa maslahi binafsi si ya taifa.
Kwa mujibu wa wawakilishi hao, wao msimamo wao ni serikali mbili na si tatu kama waraka uliotolewa na kusambazwa na watu wasiojulikana unavyodai.
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni jana, katika ukumbi wa Pius Msekwa, Katibu wa Kamati ya Wawakilishi wa CCM Zanzibar, Salmin Awadh Salmin, alisema wao hawakuhusishwa katika kutoa maoni hayo.
Salmin alisema licha ya Baraza la Wawakilishi kupata nafasi ya kutoa maoni kama taasisi, ni viongozi wachache waliobeba jukumu hilo bila kuwahusisha wengine hivyo, maoni hayo si msimamo wa baraza bali ni kikundi cha wachache.
Alisema utoaji maoni hayo ulifanyika kwa siri bila kutolewa taarifa kwa viongozi, wakiwemo wa kamati ya uongozi.
Katibu huyo alisema taarifa na maoni yaliyotolewa kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi hayakuwa na baraka au kuvishirikisha vikao husika, hivyo kubeba maoni binafsi ya viongozi waliohusika.
“Hatukuwahi kukutana au kuamua kuwasilisha maoni hayo, tunatambua labda walikuwa na nia njema kiasi cha kusahau hata utaratibu.
“Sisi wawakilishi wa CCM tutaendelea kusimamia na kutekeleza  Ilani, kanuni na miongozo ya Chama na kama Chama msimamo wetu ni serikali mbili,’’ alisema.
Salmin aliwatoa hofu viongozi na wanachama akisema wawakilishi wa CCM hawatakisaliti Chama na wanachama wake.
Alisema wao kama wana-CCM watasimamia maelekezo na miongozo kwa gharama yoyote, wakiamini Muungano imara ni wa serikali mbili. Katibu huyo aliwaasa wananchi kufuatilia kwa karibu mchakato wa katiba ili kubaini dhamira ya wapotoshaji wa malengo mema ya waasisi wa taifa la Tanzania.
“Tunaendelea kuamini kwamba, bado miongozo ya CCM ni dira pana na yenye maono ya mbali,’’ alisema.
Habari za kuamini zimesema kuwa, waraka huo ulisambazwa kwa lengo la kuvuruga Muungano na kutoa nafasi kwa wachache kutaka kuitawala Zanzibar kwa maslahi binafsi.
Pia, waraka huo umedaiwa uliandikwa na watu wachache waliojifungia na kuwa maoni yaliyomo huko hayajawahi kujadiliwa wala kupendekezwa na mjumbe wa wowote wa BLW.
Juzi, Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Sheni, alisema msimamo wa serikali mbili ndio unaokubali kwa wengi.
Pia, amesema kutokana na matakwa hayo ya wananchi, wamekubaliana kuendelea na mfumo wa serikali mbili yaani ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema uamuzi huo wa serikali mbili ulifikiwa baada ya kushauriana kati ya pande zote mbili na kwamba, chokochoko zinazoibuliwa na watu wachache kamwe hazina tija kwa watanzania.

UVCCM yambana Maalim Seif
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Zanzibar, umekitaka chama cha CUF kumbana Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad, kujiuzulu wadhifa huo.
Umesema kelele za CUF kumtaka Dk. Sheni  kubatilisha uteuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Salim Jecha Salim na kuvunja sekreteriete yake, hauna mashiko na waanza kwanza kumbana Maalim Seif.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka, alisema Maalim Seif naye ameteuliwa na Dk. Sheni hivyo, CUF wanapaswa kupigia kelele uteuzi huo badala ya Salim.
Alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Bustani huko Kiembesamaki wakati akiwashukuru wapiga kura kwa kuipa ushindi wa kishindo CCM katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo uliomalizika karibuni.
“Nimewasikia hawa jamaa zetu wanapiga kelele kutaka Salim na sekreterieti ya ZEC ivunjwe, madai yake ni ya kitoto na kipuuzi, CUF kama kimejipima na kuona kimeshindwa kabla ya mwaka 2015, kikae pembeni kwa kuwa madai yao hayana mashiko,” alisema.
Naye Mwakilishi wa Kiembesamaki Mahmoud Thabit Kombo, aliwahakikishia wananchi kuwa atafanya kila awezalo ili kukamilisha ahadi zote alizoahidi kabla ya mwaka 2015.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru