Wednesday 26 March 2014

Mgombea CUF adaiwa kumjeruhi katibu UWT

KAMPENI ZA UBUNGE CHALINZE

NA MWANDISHI WETU

WAKATI Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ikitoa tamko la kuvitaka vyama kufanya kampeni za kiungwana na kuzingatia sheria, Chama cha CUF kimeanza kutia dosari kampeni za uchaguzi jimbo la CHalinze, baada ya mgombea wake, Fabian Skauki, kumjeruhi Katibu wa UWT Kata ya Ubena, Jesca Mlimilwa.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji (mstaafu) Damian Lubuva, alisema wamefikia hatua ya kutoa tamko hilo, baada ya kuona baadhi ya vyama vimeanza kukiuka sheria.

“Katika kufuatilia kampeni hizo, NEC imebaini baadhi ya vyama vimekuwa vikitumia lugha za chuki na zisizo na staha na hata kuhamasisha wananchi kuchukua sheria mkononi au kutoa vitisho kwa wapiga kura kwa lengo la kuzuia wasishiriki uchaguzi huo,” alisema.
Habari kutoka Chalinze zilidai kuwa Skauki akiwa na wafuasi wa chama hicho walivamia ofisi ya CCM, tawi la Tukamisasa, Kata ya Ubena kwa madai ya kuwakuta na daftari la wapigakura.
Mgombea huyo ambaye alijitambulisha kuwa ofisa usalama wa taifa, alimvamia na kumtengua mkono wa kushoto katibu huyo huku wenzake wakifanya uharibifu wa vifaa vya ofisi na kuvunja vitu Mbalimbali.
Akizungumza na Jesca nyumbani kwake kijiji cha Mwidu mbele ya waandishi wa habari Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alilitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua haraka iwezekanavyo.

“Sitarajii kuendelea kumuona mgombea wa CUF uraiani kutokana na uvamizi walioufanya. CCM haitavumilia matukio ya kutumia nguvu kupiga watu na kuwateka na itahakikisha hatua zinachukuliwa.
“Tukio hili limetukera CCM...tutaongeza nguvu ya vijana wetu ili walinde viongozi wetu wa ngazi mbalimbali,” alisema Nape.
Nape alisema polisi hawatakiwi kuwa na kigugumizi ni lazima mgombea huyo akamatwe kwa kuwa hana mamlaka ya kupiga na kukamata mtu.
Jesca aliwaeleza waandishi wa habari kuwa alikuwa ofisini na wenzake akamuona Skauki akiingia ofisi kwake na kumuuliza kwa nini ana orodha ya wapiga kura kwani itasababisha akose kura.
 Alisema wengine hawatambui lakini yeye alimpiga na kumnyonga mkono ambao sasa umefungwa plasta gumu.
Alisema baada kumpiga alimkamata na kumpakia kwenye gari lake na kumpeleka Kituo cha Polisi Mdaula.
Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani, Sauda Mpambalyoto, alisema kabla kuanza kampeni vyama vyote vilikutana na kamati ya ulinzi na usalama na kusaini makubaliano ya kufanya kampeni za kistaarabu lakini CUF imeanza kukiuka.
 Mratibu wa Uchaguzi wa Kata ya Ubena na Katibu wa CCM wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu, amelaani kitendo hicho na wamefungua kesi wakitaka pamoja na mambo mengine CUF ifidie uharibifu iliyoufanya.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Samuel Sarianga, alisema si kosa kuwa na orodha ya wapiga kura kwa kuwa vyama vyote vilipewa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema anafuatilia tukio hilo na kwamba hatua zitachukuliwa.
Akifafanua Jaji Lubuva alisema tangu kuzinduliwa kwa kampeni  za uchaguzi jimboni humo Machi 13, mwaka huu, NEC imekuwa ikifuatilia kampeni katika maeneo mbalimbali ya jimbo na vyama vilivyosimamisha wagombea kwa kuzingatia ratiba iliyowekwa na Msimamizi wa Uchaguzi baada ya kushauriana na vyama husika.
Jaji Lubuva alisema NEC inakemea kwa nguvu na kulaani vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya wanasiasa na kutaka ikumbukwe matumizi ya lugha za kejeli, vitisho na kuzuia wapiga kura kushiriki uchaguzi ni ukiukwaji wa sheria.
Alionya kwamba kwa yeyote atakayebainika kukiuka na kuvunja sheria atachukuliwa hatua kali na atakayeshukiwa kufanya vitendo hivyo akabidhiwe kwenye vyombo vya sheria na si kuchukua sheria mkononi.

“Tume inatarajia kuona kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura jimboni humo anatumia haki yake ya kikatiba na sheria ya kupiga kura kwa amani na utulivu, pasipo vitisho wala kubugudhiwa,”aliongeza.
Wananchi  wa Chalinze watapiga kura kumchagua mwakilishi wao Aprili sita mwaka huu, na uchaguzi huo unafanyika kuziba nafasi iliyoachwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo, aliyefariki dunia hivi karibuni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru