Tuesday 4 March 2014

Sitta, Samia waamsha shangwe bungeni


NA WAANDISHI WETU, DODOMA

WAKATI mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, akipigiwa chapuo kiaina kuwania uenyekiti wa bunge hilo, Samia Suluhu Hassan, amesema kuongoza bunge hilo si changamoto kwake kutokana na uzoefu alio nao.

Samia Suluhu Hassan

Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza jana kuhusu uwasilishaji wa taarifa ya wajumbe walio wachache bungeni, alisema watu wanaweza kuwa na wasiwasi na mwenyekiti atakayewasilisha taarifa hizo kwamba anaweza kuwaburuza.
Alisema wanahitaji kupata muafaka na kwamba mwenyekiti anaweza kuwa mawazo yake ni katika kundi la wachache lakini atawajibika kutoa taarifa yote ya kamati na hasa ikiwa katika mchakato wajumbe watampata mwenyekiti anayesimamia viwango.
Kauli ya Profesa Lipumba ilipokewa na wajumbe kwa kofi na nderemo, ikiashiria kumlenga Sitta, ambaye wakati wa uongozi wake akiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kaulimbiu yake ilikuwa viwango na kasi.
Samia kwa upande wake, akijibu maswali ya waandishi wa habari jana mjini hapa, kama ana uwezo wa kuongoza bunge hilo, alisema hadhani kama hiyo ni changamoto kwake kutokana na uzoefu alio nao.
“Nadhani uongozi wa Bunge la Katiba ni wa muda mfupi kuliko kupewa wizara na ukaiendesha. Nimeshakuwa Waziri wa Ajira, Vijana, Wanawake na Watoto Zanzibar kwa miaka mitano; Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji Zanzibar kwa miaka mitano na katika Wizara ya Muungano huu ni mwaka wangu wa nne, bila hata kusikia kutikiswa huku au huku,” alisema.
Samia aliongeza: “Ikiwa nimeyaweza yote hayo, mengine yanayokuja sidhani kama ni changamoto kwangu.”
Juzi, wabunge wa CCM walimpitisha Sitta kwa kauli moja kuwania nafasi hiyo na kwamba, duru zinaonyesha amekuwa akiungwa mkono hata na wapinzani kutokana na uwezo wake na mahiri wa kuongoza bunge lililopita.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru