Tuesday 25 March 2014

Wanachama wapeleka kilio CHADEMA


WAKATI kampeni zikishika kasi jimbo la Chalinze, baadhi ya wanachama na viongozi wa CHADEMA wamekitosa chama hicho.
Viongozi walioihama CHADEMA na kujiunga CCM ni Katibu wa kata ya Msata, Mrisho Issa, Katibu wa Uhamasishaji, Nasibu Msakamali na  mjumbe Subira Mrisho.
Kwa nyakati tofauti walikabidhi kadi zao za CHADEMA kwa viongozi wa CCM kwenye mikutano ya kampeni jimboni Chalinze.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akiwapokea baadhi ya wanachama hao wapya alisema wamefanya uamuzi sahihi.
Mgombea wa CCM, Ridhiwani Kikwete, alikabidhi kadi kwa vijana 40 katika mashina ya wakereketwa waliojiunga na Chama na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Akizungumza na vijana wa Pongwe Kiona, aliahidi akiwa mbunge atahakikisha wanawezeshwa ili kupiga hatua katika maendeleo.
“Natambua shida zenu, naomba mjiunge pamoja kwenye vikundi ili mnufaike na asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya kinamama na vijana,” alisema.
Alisema CCM imetoa heshima kubwa kwa vijana kwa kumteua kugombea ubunge, hivyo hawezi kuwaangusha, ikizingatiwa vijana ndio nguvu kazi ya taifa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru