Wednesday 5 March 2014

Mafuriko yaikumba hospitali Dar

NA MWANDISHI WETU

HOSPITALI ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni ya Sinza Palestina, imekumbwa na mafuriko na kusimamisha kazi kwa muda, kutokana na mvua zilizonyesha jana.
Mafuriko hayo yalisababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyakazi na wagonjwa waliofika kupata matibabu, baada ya maji machafu kutanda eneo lote la hospitali hadi katika baadhi ya wodi na kusababisha kutopitika. 
Uhuru lilishuhudia wauguzi wakiacha kazi na kupanda juu ya meza na viti wakiyakwepa maji hayo, na wengine kukimbia katika eneo hilo kuhofia kusombwa na maji hayo.
Maji hayo ambayo hayakuwa ya mvua pekee, bali yalichanganyika na maji taka ya vyoo, yalilifanya eneo hilo kuwa na uchafu wa aina yake.
Baada ya mvua hiyo kwisha, iliwalazimu wafanya usafi wachukue muda wa zaidi ya dakika 30 kuondoa uchafu na tope lililokuwa limejaa karibu vyumba vyote vilivyo eneo la chini.
Hali ya mafuriko katika hospitali hiyo pia inachangiwa kwa kiasi kikubwa na chemba zilizopo,  ambapo pindi mvua inaponyesha zinafurika na kusambaza maji machafu.
Baadhi ya wagonjwa ambao wengine walikuwa katika hali mbaya, wameiomba serikali iangalie tatizo hilo maana licha ya maji hayo kuwa mengi, pia ni hatari kwa afya zao kwa ujumla.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru