Tuesday 18 March 2014

Usafirishaji Meno ya tembo Mchina jela miaka 20


NA FURAHA OMARY
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Mhandisi Yu Bo (45), raia wa China, kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya sh. bilioni tisa, baada ya kutiwa hatiani kwa kupatikana na nyara za serikali.


Yu, mkazi wa Masaki, Dar es Salaam, alikiri kosa la kupatikana na meno ya tembo yenye thamani ya sh. milioni 975 na magamba ya kakakuona, nyara alizokuwa katika harakati ya kuzisafirisha kwenda China.
Hakimu Mkazi Devotha Kisoka, alitoa hukumu hiyo jana, baada ya mshitakiwa kukiri kosa na maelezo ya awali.
Yu alikiri kosa juzi, baada ya kusomewa hati ya mashitaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi Faraja Nchimbi.
Nchimbi alimsomea shitaka baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashitaka dhidi ya Nasaro Juma (29), mkazi wa Sinza, ambaye ni dereva aliyeshitakiwa pamoja na Yu.
Yu alikiri kukamatwa Desemba 30, mwaka jana, katika Bandari ya Dar es Salaam, eneo la Temeke akiwa na vipande 81 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 303 na thamani ya sh. 975,076,350.
Pia alikiri kupatikana na magamba 130 ya kakakuona, yenye thamani ya sh. 3,044,140. Nyara hizo za serikali zina thamani ya sh. 978,120,490, ambazo alipatikana nazo bila kuwa na kibali au leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Baada ya kukiri kosa, Nchimbi alimsomea maelezo ya awali akidai Yu alikamatwa akiwa katika harakati za kusafirisha nyara hizo kwenda China, ambayo aliyakubali.
Hadi jana mchana Yu hakuwa amelipa faini, hivyo alipelekwa jela.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru