Thursday 13 March 2014

JK mbioni kufungua Bunge


NA CHARLES MGANGA, DODOMA 
KATIBU wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Thomas Kashililah, amesema Rais Jakaya Kikwete atalizindua Bunge Maalumu la Katiba baada ya wajumbe wa Bunge hilo kuapishwa.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Dk. Kashililah alisema Rais atazindua Bunge hilo baada ya utaratibu unaoendelea kukamilika.
“Kwa kweli siku rasmi ya Rais kuzindua Bunge la Katiba ni mpaka taratibu zinazoendelea kukamilika ikiwa ni pamoja na kazi ya kuapa kwa wajumbe hao,” alisema kiongozi huyo wa Bunge.
Alisema baada ya kumalizika uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, kazi itakayofuata ni kuapishwa kwa makatibu ambao watakuwa na jukumu la kuwaapisha Mwenyekiti na Makamu wake.
Uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Bunge, unatarajiwa kufanyika kesho jioni baada ya wajumbe wanaowania nafasi hiyo kujitokeza.
“Kesho (leo), jioni tutafanya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu kabla ya wao kuapishwa na Katibu.
“Wakishaapishwa wao, hatua itakayofuata ni Mwenyekiti kuanza kuwaapisha wajumbe mmoja baada ya mwingine,” aliendelea kufafanua.
Wajumbe waliomo kwenye bunge maalumu la katiba ni 629, wakiwemo Wabunge wa Muungano, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wajumbe 201 walioteuliwa na Rais kutoka katika makundi mbalimbali.
Aidha, Katibu huyo wa Bunge alisema kazi ya kuwaapisha wajumbe wote huenda ikachukua siku mbili na nusu.
“Unajua tumefanya hesabu, mjumbe mmoja atatumia dakika mbili au tatu kuapa, sasa kazi hiyo inaweza kutumia kama siku mbili na nusu mpaka kumaliza,” alisema Kashililah.
Juzi, wajumbe hao wa Bunge la Katiba, walipitisha kanuni ambazo zitawaongoza wakati wa kuijadili rasimu ya katiba.
Kanuni hizo zilipita kwa kishindo baada ya Kamati ya Kanuni iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba Pandu Ameir Kificho kuiteua ikiwa chini ya Profesa Costa Mahalu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru