Thursday 13 March 2014

Polisi majambazi hadharani kesho


Na mwandishi wetu
POLISI Mkoa wa Kinondoni, Dar es Salaam, imekiri baadhi ya askari wanashirikiana na majambazi, ambao majina yao yatawekwa hadharani kesho.
Licha ya majina, hatua zitakazochukuliwa dhidi yao pia zitaanikwa.
Askari hao imeelezwa wanatoka makao makuu ya Jeshi la Polisi na maeneo mengine ya utendaji wa polisi jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Camillius Wambura, baadhi ya askari wamehusika na tukio la uporaji kwenye ofisi ya Hong Yang, inayomilikiwa na raia wa China, iliyoko Mbezi Beach.
Tukio hilo lilitokea Machi 9, mwaka huu, saa nne usiku, ambapo majambazi 15 yalivamia ofisi hiyo ya useremala na ujenzi wa nyumba na kupora simu ya iphone yenye thamani ya dola za Marekani 400 (sh. 660,000), funguo za gari aina ya Toyota Harrier namba T 866 BVX, sh. milioni moja na simu ya mkononi aina ya Oking, yenye thamani ya sh. 20,000.
Kamanda Wambura akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu uporaji huo, alisema watuhumiwa wanne wanashikiliwa, ambao walishirikiana na askari wa Jeshi la Polisi wasio waaminifu.
Aliwataja kuwa Gerard Matutu (36), mfanyabiashara wa vyuma chakavu na mkazi wa Temeke, Charles Mbelwa (37), fundi magari anayeishi Kurasini, Adam Mohamed (44) mkazi wa Kariakoo na Ally Salum (38) wa Vingunguti.
“Uchunguzi wa kina unaendelea, taarifa kamili juu ya ushiriki wa askari hao itatolewa Ijumaa, ikiwa ni pamoja na hatua zitakazokuwa zimechukuliwa,” alisema.
Kamanda Wambura alisema kukamatwa kwa watuhumiwa kunatokana na taarifa ya raia wema na askari wa Kampuni ya KK Security, ambao baada ya kusikia kelele walikwenda eneo la tukio.
Alisema walikamatwa wakiwa na mapanga, nondo, bastola na gari namba T 664 AFF, aina ya Toyota Mark II.
Tukio hilo si la kwanza la askari polisi mkoani Dar es Salaam, kutuhumiwa kushiriki vitendo vya uhalifu.
Mei, mwaka jana, askari 16 walikamatwa wakituhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara ya magendo, wanaovusha bidhaa kupitia ‘bandari bubu’ zilizo kando mwa Bahari ya Hindi, kuanzia eneo la Kawe hadi Bagamoyo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema askari hao walishirikiana na wafanyabiashara ambao walitoa rushwa ili wasikamatwe, jambo ambalo lililidhalilisha Jeshi la Polisi na kuikosesha serikali mapato.
Polisi pia walihusishwa katika tukio la kuvamia na kupora fedha katika Benki ya Habib African Ltd, iliyoko mtaa wa  Livingstone na Uhuru, Kariakoo.
Tukio hilo lilitokea Agosti 29, mwaka jana, ambapo moja kati ya majambazi hayo lilikuwa limevaa sare za Jeshi la Polisi na yalikuwa na gari aina ya Toyota Noah namba T 817 BPZ.
Desemba 17, mwaka 2012, Polisi pia walituhumiwa kutokomea na sh. milioni 150 za Kampuni ya Artan Ltd, zilizoporwa katika tukio la ujambazi uliofanyika Kariakoo.
Kamanda Kova akizungumzia tukio hilo, alikiri polisi kuhusika na Machi 10, mwaka jana, aliwataja askari waliohusika kuwa Sajini Dancan, Koplo Rajab, Koplo Calvin, Koplo Geofrey na Koplo Kawanami.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru