Tuesday 25 March 2014

Wabunge wajipanga kumng’oa Spika EAC



  • Wakerwa kumruhusu mumewe kuhudhuria Bunge
  • Rais Kenyatta atua kutuliza hali ya hewa, awasihi 

NA LILIAN JOEL, ARUSHA
WABUNGE wa Bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki (EALA) leo wamepanga kumng’oa Spika wa bunge hilo, Dk. Margerth Ziwa, wakimtuhumu kwa mambo mbalimbali, ikiwemo dharau.
Wakizungumza na Uhuru baada ya Mwenyekiti wa Jumuia hiyo ambaye ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kuhutubia Bunge hilo, baadhi ya wabunge walisema wamekuwa wakililalamikia kwa muda mrefu mume wa Spika huyo waliyemtaja kwa jina moja la Babu kuhudhuria vikao vya bunge kama mbunge, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za bunge hilo.
Pia walilalamikia kitendo cha Spika kuwaajiri baadhi ya ndugu zake kwa kuwapa mikataba ya muda mfupi ya kufanya kazi kwenye bunge huku kukiwa na watu wengine wenye uwezo ambao hawapewi nafasi hizo.
Wabunge hao kutoka karibu nchi zote wanachama, walisema kipindi cha mashindano ya mpira wa  mabunge ya nchi wanachama yaliyofanyika  Uganda hivi karibuni, Spika huyo aliwapeleka wananchi wa kawaida kuchezea timu ya bunge la Uganda kama wabunge.
“Ni kweli leo lazima tumgo’oe spika kwa kuwa ameshindwa kufikia viwango vya kiutendaji na anatudharau wakati sisi tumepewa dhamana na nchi zetu kwa ajili ya maslahi ya Jumuia nzima na si mtu binafsi,” alisema mmoja wa wabunge hao.
Hata hivyo, mmoja wa wabunge hao ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, aliliambia Uhuru kuwa Mwenyekiti wa Jumuia hiyo, alimsihi mwenyeviti wa wabunge kutoka nchi wanachama kuzungumza nao ili wasimng’oe.
Akizungumza kwa lugha ya Kiingereza alisema: “Waandishi huko ndani Mwenyekiti wa Jumuia anamuombea spika aendelee kubaki kwenye nafasi yake lakini  sisi hatuko tayari kuendelea kufanya kazi naye. Kazi  ya kwanza tukayoifanya kesho (leo) kabla ya bunge kuanza ni kuhakikisha tunamng’oa.
“Kuong’olewa kwa spika ni mkakati wa wabunge wote hapa hakuna cha Mganda wala Mtanzania. Hili  ni jambo ambalo tumeazimia kwa pamoja kuwa lazima aachie nafasi hiyo ndipo kikao cha bunge kiweze kuendelea.”
Alisema kuna watu wenye uwezo wa kuongoza bunge hilo ambao ni wasikivu na kwamba hawaoni shida kumg’oa katika nafasi hiyo kwa ajili ya kumuweka mtu mahiri anayechukua ushauri anaopewa na wabunge.
Mkutano huo wa tano na kikao cha pili cha bunge hilo, kinafanyika katika ukumbi wa Bunge uliopo kwenye ofisi za Makao Makuu ya EAC kwa wiki mbili.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru