Wednesday 12 March 2014

Sendeka: Serikali tatu hazitamaliza matatizo


NA CHARLES MGANGA, DODOMA
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Christopher Ole Sendeka, amesema yeye ni muumini wa serikali mbili.
Akizungumza baada ya Wajumbe wa Bunge kupitisha kanuni ambazo zimefanyiwa marekebisho, Ole Sendeka alisema suluhisho la matatizo ya nchi si kuongeza serikali.


Sendeka ambaye pia ni Mbunge wa Simanjiro (CCM), alisema jambo la msingi ni kuhakikisha changamoto hasa zinazohusu muungano zinapaswa kufanyiwa kazi na si kuongeza idadi ya serikali.
“Pamoja na kwamba ni mwanachama wa CCM, binafsi ni muumini wa serikali mbili. Jambo linalopaswa kufanywa kwa sasa ni kuhakikisha dosari zinaondolewa.
“Hata kama serikali zitaongezeka, si suluhu ya matatizo yaliyopo nchini. Kwa kawaida hata kama zingekuwa hizo serikali tatu ambazo baadhi ya wengine wanataka, si kweli kama tutafikia kule tunakokutaka,” alisema.
Alisema wananchi wangependa kuona matatizo yanayowakabili ikiwa ni pamoja na barabara, maji, reli na miundombinu yote kwa ujumla ikipatiwa ufumbuzi.
Aidha, Sendeka alisema kwa sasa kazi ya Bunge Maalumu la Katiba si kushughulikia changamoto hizo, isipokuwa kuhakikisha nchi inapata katiba nzuri ambayo itasaidia kuifikisha Tanzania katika mafanikio.
“Hili Bunge kazi yake kubwa ni kuhakikisha Tanzania inapata katiba mpya, ni vyema busara ikatumika ili wananchi wote kwa ujumla wanufaike,” aliongeza.
Jana, Bunge hilo Maalumu la Katiba lilikubaliana kwa pamoja kupitisha kanuni ambazo zitawaongoza katika shughuli zao za kujadili rasimu ya katiba.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru