Tuesday 25 March 2014

Sitta apangua mitego mikali


NA LILIAN TIMBUKA, DODOMA
MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, jana alipangua hoja za mtego kuhusu uteuzi wa wenyeviti wa kamati za maridhiano za bunge hilo.


Wajumbe hao, asilimia kubwa kutoka Zanzibar na wale wa vyama vya upinzani, walionyesha hofu, ambayo ilitulizwa na Sitta baada ya kufafanua kuwa, uchaguzi lazima uzingatie Kanuni ya 55 (1).
Kwa mujibu wa wajumbe hao, kutokana na idadi iliyopo ambayo inautofauti kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa na wajumbe wengi ndani ya bunge, huenda wenyeviti wengi wakatoka katika Chama au Tanzania Bara.
“Sioni sababu ya ninyi kuwa na hofu, kinachoongoza hapa ni kanuni ambayo inapaswa izingatiwe; na imeeleza wazi, kama mwenyekiti atatoka Bara, makamu atatoka Zanzibar na inaeleza pia tuzingatie jinsia,” alisema Sitta.
Licha ya majibu hayo, baadhi ya wajumbe waliendelea kuomba mwongozo wakihoji suala hilo.
Sitta alisema uchaguzi hauwezi kubeba dhana za wajumbe wanazozifikiri bali utafuata sheria na kanuni, hivyo kila mjumbe ana haki ya kugombea katika kamati bila kujali anatoka kundi gani au jinsia.
“Nadhani mkifuata mwongozo wa kanuni mtafika kule mnakotaka kufika, na hofu hizi mlizoanza kuzionyesha zitaisha,” alisema.
Sitta alisema kamati zilizoundwa jana zinatarajiwa kuanza kazi ya kuchambua Rasimu ya Pili ya Katiba, Ijumaa wiki hii.
Alisema baada ya uchaguzi kukamilika, leo atatangaza majina ya viongozi wa kamati hizo na za Uandishi, Kanuni na Maadili.
Mwenyekiti alisema leo itaundwa Kamati ya Uongozi inayotokana na wenyeviti wa kamati zote. Kamati 12 za Maridhiano zenye wajumbe kati ya 52 na 53 kila moja zimeundwa, huku Kamati za Kanuni na Haki za Bunge na ya Uandishi, zikundwa na wajumbe 24 kila moja.
Sitta alisema uteuzi wa wajumbe katika kila kamati umezingatia uwiano wa wajumbe na jinsia na kwamba, wajumbe wa Kamati ya Uandishi na ya Kanuni na Haki za Bunge, ni wajumbe kwenye kamati zingine.


Hotuba za JK, Jaji Warioba kutikisa
Hotuba zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, zinatarajiwa kujadiliwa kesho bungeni.
Akijibu ombi lililotolewa na Julius Mtatiro, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Sitta alisema muda umetengwa wa kuzijadili hotuba hizo.

Mtatiro aliomba mwongozo kuomba hotuba hizo zijadiliwa kabla ya kazi za kamati hazijaanza ili kuondoa minong’ono inayoendelea miongoni mwa wajumbe.
“Mwenyekiti naomba mwongozo wako katika hili, binafsi naona ni vyema hotuba hizi mbili za Rais na ya Jaji Warioba, zijadiliwe na wajumbe kabla hawajaanza kazi,” alisema.
Alisema kuna dhana imejengeka miongoni mwa watu kuwa Rais Kikwete alijibu hotuba ya Jaji Warioba.
“Ili kuondoa haya yote, unaonaje na Jaji Warioba naye akaitwa tena aje ajibu kile kilichoelezwa na Rais,” alisema.
Sitta alisema haiwezekani akaitwa tena bungeni, bali kitakachofanyika ni kwa wajumbe kupewa muda wa kuijadili.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru