Thursday 13 March 2014

Sitta atoa ya moyoni juu ya Muungano


NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
MWENYEKITI mteule wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, amesema atawashughulikia watu wachache wasiotaka Muungano.


Sitta, ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na mbunge wa Urambo Mashariki, alisema hayo juzi, alipotoa shukrani kwa wajumbe waliomchagua kushika wadhifa huo.
Alisema kuna wajumbe wachache wenye nia ya kuuvunja Muungano, hivyo busara zitatumika kuhakikisha hilo halifanikiwi.
“Kuna wachache hawataki Muungano, hao tutashughulika nao. Busara zipo za kutosha za kushughulikia hilo,” alisema.
Alisema angependa Muungano uendelee kuwepo kutokana na faida zilizopo kwa wananchi wa pande zote mbili.
“Nawashukuru wajumbe kwa kunichagua, kuna wajumbe wawili au watatu katika maelezo na michango yao wameonyesha dhamira ya kuuvunja Muungano hawa nitashughulika nao kikamilifu.
“Nawaahidi kufanya kazi kwa uadilifu, kasi na uzalendo katika kuhakikisha inakamilika kwa wakati,” alisema.
Alisema atahakikisha katiba nzuri inapatikana, ambayo itawarejeshea wananchi imani kwa serikali. Aliwataka Watanzania watarajie katiba yenye kulinda na kusimamia haki zao.
Sitta alisema katika mchakato wa kugombea nafasi hiyo mambo mbalimbali yalitokea, ikiwemo baadhi ya watu kueneza uzushi kuwa na ugomvi na mjumbe Andrew Chenge.
“Katika mchakato kama huu wanakuwepo wapambe, hawa wanaeneza mambo hata ya wongo ndiyo maana wakaitwa wapambe nuksi.
“Mimi na Chenge tuna historia ndefu hata kuwa mwanasheria mkuu, nilipendekeza jina lake kwa Rais wa awamu ya pili (Ali Hassan Mwinyi) sasa sijui huo ugomvi umetoka wapi,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru