Wednesday 26 March 2014

Ridhiwani ahadharisha wawekezaji

KAMPENI ZA UBUNGE CHALINZE

NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA wa Ubunge wa CCM, Ridhiwani Kikwete, ametangaza vita dhidi ya wawekezaji katika machimbo ya kokoto waliongia mikataba ya kinyonyaji na kusababisha migogoro na wananchi.
 Amesema akiwa mbunge hatavumilia kuona wananchi wakinyonywa na wawekezaji kutokana na mikataba mibovu inayowaneemesha binafsi na kuwaacha wananchi katika hali ngumu.
Ridhiwani alisema hayo jana alipozungumza na wananchi katika mikutano ya kampeni za uchaguzi zinazoendelea katika jimbo hilo.


“Hatuhitaji wawekezaji wa kututia umasikini...wananchi wana haki ya kunufaika na matunda ya uwekezaji na si kama ilivyo sasa ambapo hata ajira kwa vijana imekuwa taabu,” alisema  Ridhiwani ambaye ni mwanasheria.
Alisema akichaguliwa kuwa mbunge atahakikisha mikataba yote inapitiwa upya na kuweka utaratibu mzuri ambao wananchi watanufaika.
Mgombea huyo, alisema wapo wawekezaji wamekumbatia maeneo makubwa ya ardhi bila ya kuyandeleza wakati wapo wenye uwezo wa kuyaendeleza kwa faida ya jamii.
Akizungimzia kero hiyo, Diwani wa Kara ya Lugoba, Rehema Mwene, alisema wawekezaji wengi wanakiuka utaratibu wa kusaidia huduma za jamii kwenye maeneo waliyowekeza. 
Alisema wanashindwa kushirikiana na vijiji kuboresha miundombinu wakati magari yao makubwa yanayobeba hadi tani 30 yanapita kwenye barabara hizo na wengine waliochukua vijana wachache wanashindwa kuwalipa mishahara kwa wakati.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru