Tuesday 4 March 2014

Sitta Mwenyekiti Bunge la Katiba

NA MWANDISHI WETU

  • Wajumbe CCM wampitisha kwa kauli moja
  • Chenge ajitoa, Samia Suluhu makamu wake

SPIKA mstaafu Samuel Sitta anatarajiwa kuongoza Bunge Maalumu la Katiba, baada ya maridhiano mbalimbali miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kutokana na maridhiano hayo, Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki na Waziri wa Afrika Mashariki, atakuwa mgombea pekee wa nafasi wa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika jana, zimesema kuwa Sitta alitipitishwa kwa kauli moja baada ya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kutangaza kuondoa jina lake kwa hiyari mwenyewe.
Chenge ni miongoni mwa makada wa CCM waliokuwa wakitajwa kuwania nafasi hiyo, ambapo jana aliwaeleza wajumbe kuwa anaondoa jina na kumwachia Sitta nafasi ya kuwania nafasi hiyo.
Habari zaidi zimeeleza kuwa Sitta, ambaye ameweka historia katika uongozi wake wa Bunge la 10 kutokana na falsafa yake ya Viwango na Kasi ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko makubwa katika taasisi hiyo hivyo, kujijengea heshima ndani na nje.
Pia, anaungwa mkono na wabunge wengi wa CCM na kwamba, kutokana na hilo kuna dalili kubwa kwa wapinzani kutosimamisha mgombea kuchuana na Sitta kutokana na heshima aliyojijengea katika uendeshaji wa taasisi hiyo.
Habari zaidi zilisema jina la Sitta lilipochomoza kuwa ndiye atakayewania nafasi hiyo, shangwe zilitawala kikao hicho ambapo, tayari mwenyewe aliwahi kukaririwa akieleza kuwa amejipanga kikalimifu katika kuendesha Bunge hilo la kihistoria na kusaidia taifa kutimiza malengo ya kupata Katiba bora na inayokidhi matakwa ya wengi.
Mbali na Sitta, katika kikao hicho wabunge walipitisha jina la Samia Suhulu Hassan kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo. Samia, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), naye alionekana kuungwa mkono na wabunge wengi.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru