Sunday 2 March 2014

Ikulu: Hakuna mbunge aliyeongezewa posho



  • JK aridhia marekebisho mengine, posho kuendelea kuwa sh. 300,000
Na Mwandishi wetu
MJADALA wa nyongeza ya posho kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, umefungwa rasmi baada ya Ofisi ya Rais Ikulu, kusema kiwango cha posho kitaendelea kuwa sh. 300,000 kwa siku.
Pia, imesema hakuna mbunge aliyeongezewa posho na kuwa, hakuna maombi yaliyowasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete kuombwa kuaridhie nyongeza ya viwango vya posho kutoka sh. 300,000 hadi 500,000.
Kutokana na hatua hiyo, Ikulu imesema hakuna ongezeko lolote la posho za wajumbe ambalo, Rais Kikwete ameliridhia na kutaka mjadala huo ufungwe kwa kuwa hauna tija wala ukweli.
Hivi karibuni baadhi ya wajumbe wa bunge hilo limbana Mwenyekiti wa Bunge, Pandu Ameir Kificho wakidai posho ya sh. 300,000 wanayolipwa kwa siku ni ndogo na hailingani na gharama za maisha ya Dodoma.
Madai hayo yalimlazimu Pandu kuunda Kamati kwa ajili ya kufuatilia posho ambayo iliundwa na wajumbe sita akiwemo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Wengine ni Mohammed Aboud Mohammed, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Paul Kimiti, Asha Bakari Makame, ambaye amewahi kushika nyadhifa za uwaziri Zanzibar na Jenista Mhagama, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Hata hivyo, madai hayo yalizusha mjadala mkali kutokana na wananchi kupinga na kuwatuhumu wabunge kujali maslahi yao mbele badala ya kazi waliyotumwa.
Pia, baadhi ya wajumbe walipingana na wenzao kuhusu nyongeza hiyo na kueleza kuwa kiasi wanacholipwa kwa siku ni kikubwa.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu kwa vyombo vya habari jana, imesema kuwa Rais Kikwete hajapokea maombi kutoka kwa Uongozi wa Bunge kumwomba aridhie posho mpya hivyo, wajumbe wote watalipwa sh. 300,000 kwa siku.
Imesema kuwa kumekuwepo na habari nyingi, baadhi zenye kuchanganya umma kuhusu posho za wajumbe wa Bunge la Katiba.
Imesema kuwa taarifa zingine zimedai kuwa baadhi ya wafanyakazi nchini wamepanga kuandamana iwapo Rais Kikwete, atakubaliana na maombi ya nyongeza ya posho hizo.
‘’Mhe. Rais hajapata kupokea maombi yoyote kutoka kwa Uongozi wa Bunge ya kumwomba aridhie kuongezwa kwa posho ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kiwango cha sasa cha sh. 300,000 kwa siku hadi kufikia 500,000 ama 700,000 kama ambavyo imekuwa ikivumishwa.
‘’Mhe. Rais hajapata kupokea maombi ya nyongeza ya posho hiyo, hakuna ongezeko lolote la posho ambalo Mhe. Rais ameliidhinisha.
‘’Kwamba alichopokea Mhe. Rais ni maombi ya Uongozi wa Bunge wa kuomba Mhe. Rais aridhie kufanyika marekebisho katika kiwango cha malipo ya siku kwa wajumbe hao cha sh. 300,000 ili posho ya kikao iwe posho ya kujikimu na posho ya kujikimu iwe ndio posho ya kika,’’ ilisema taarifa hiyo.
Pia, imeongeza kuwa Rais Kikwete amelikubali ombi hilo la kufanyika kwa marekebisho katika mpangilio huo wa posho, lakini kiwango cha malipo ya kila siku kitaendelea kuwa sh. 300,000 kwa siku.
WAJUMBE WAJA JUU
Akizungumzia hilo, mjumbe James Mbatia, ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema suala la posho halina umuhimu katika katiba, bali cha muhimu ni kupata katiba bora.
Kwa upande wake, mjumbe Issa Ameir Suleiman, alisema suala la posho limezuka kutoka kwa baadhi ya wajumbe lakini halina nafasi.
Alisema baadhi ya wajumbe katika maeneo yao hawapati kiwango hicho cha posho wanapokwenda kwenye shughuli kama vile makongamano.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema serikali haina fedha za nyongeza kwa posho za wajumbe na kwamba, anayeona sh. 300,000 haimtoshi ni vyema akafungasha virago.
Alisema serikali ina mambo mengi ya kufanya kwa ajili ya maendeleo ya watanzania na kwamba, haiwezi kutumia mamilioni ya shilingi kulipa wajumbe wa bunge hilo.
‘’Kama taifa tuna matatizo mengi na mambo muhimu ya kufanya, hatuwezi kulipa wajumbe posho ya sh. 500,000 kwa siku, kama kuna aliyeona kiasi hicho hakimtoshi afungashe virago aondoke Dodoma,’’ alisema Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara).

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru