Tuesday 25 March 2014

Wafanyakazi Shoprite wagoma


NA JUMANNE GUDE
WAFANYAKAZI wa maduka ya Shoprite ya jijini Dar es Salaam, wamegoma kuendelea na kazi wakishinikiza mwajiri awalipe stahili zao kabla ya kukabidhi kwa mmiliki mpya.
Taarifa kutoka ndani ya kampuni hiyo, zinasema maduka hayo ambayo ni maarufu kwa kuuza bidhaa mbalimbali, yameuzwa kwa mwekezaji mwingine na kwamba wafanyakazi wake bado hawajalipwa malipo mbalimbali hivyo kuamua kuingia kwenye mgomo.
Mgomo huo ulianza jana saa mbili asubuhi katika duka la Kamata, ambapo wafanyakazi wakiwa na mabango walilipuka na kuanza kushinikiza kulipwa fedha za likizo na matibabu.
Msemaji wa wafanyakazi hao, Bahati Kalolo, alisema mwajiri huyo amekuwa mkaidi kuwalipa haki zao na kwamba hata alipoitwa katika Baraza la Usuluhishi hakutokea.
Kalolo alisema wanamdai mwajiri wao huyo zaidi ya miaka minane, lakini haelekei kuwalipa na kwamba maduka hayo yameshauzwa kwa mmiliki mwingine.
Alisema wamefuatilia suala hilo hadi Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), lakini hakuna msaada waliopewa, hivyo kulazimika kuingia kwenye mgomo ili kushinikiza kupata ufumbuzi wa suala hilo.
“Hatufahamu huyu jamaa anataka kutuacha vipi, maduka haya yameshauzwa kwa raia wa Kenya na wiki ijayo atakabidhiwa lakini mpaka sasa hatujalipwa haki zetu,” alisema.
Mfanyakazi mwingine, Mohamed Athumani, alisema wanamtaka mwajiri huyo kutengeneza jedwali la kila mfanyakazi litakaloonyesha kiasi atakacholipwa.
Athumani alitoa ushauri kwa serikali kuwa wawe makini na wawekezaji wanaokuja nchini kutokana na tabia ya kuwanyanyasa wafanyakazi wazawa na kuhakikisha haki zao zinapaitkana.
Hata hivyo, waandishi walipomfuata mmiliki wa Shoprite, ili aweze kuzungumzia madai hayo, walifungiwa ndani ya chumba na badala yake askari ndio walioruhusiwa kuingia ndani kwa mwajiri huyo


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru