Thursday 13 March 2014

Vigogo CHADEMA waitosa Kalenga



  • Wahaha kumnusuru Mchungaji Msigwa

NA SULEIMAN JONGO, Iringa
UPEPO mbaya katika uchaguzi mdogo wa ubunge Kalenga, umezidi kuvuma katika kambi ya CHADEMA, ambayo  imeamua kukimbia jimboni humo.
Chama hicho kimehamishia kampeni Iringa Mjini, ambako viongozi wakuu wa chama hicho, wakiwemo wabunge wamekuwa wakizunguka wakidai kusaka kura.
CHADEMA jana ilifanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mwembe Togwa, Manispaa ya Iringa, ambako pamoja na mambo mengine ilihamasisha kuchaguliwa kwa chama hicho Kalenga.
Mkutano huo ulifanyika siku chache baada ya helikopta ya chama hicho kusambaza vipeperushi vya kumnadi mgombea wa CHADEMA katika uchaguzi huo, Grace Tendega.
Habari za kuaminika zinasema viongozi hao wameikimbia Kalenga na wanafanya mikutano ya hadhara ili kumnusuru mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, ambaye ana hali mbaya kutokana na wananchi kumkataa.
Akizungumzia mkutano huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, alisema ni mwendelezo wa kuchanganyikiwa kwa chama hicho baada ya kuona upepo mbaya ukivuma kwa mgombea wao Kalenga.
“Hii ni ajabu, hivi unapata wapi muda wa kufanya mkutano Iringa Mjini wakati huu tukiwa kwenye wiki ya mwisho ya kampeni. Tuna taarifa kutoka CHADEMA zinazosema wamekata tamaa ya kushinda, hivyo wanachofanya ni kutafuta namna ya kujitetea,” alisema.
Alisema CHADEMA imeona dalili za kushindwa hivyo inabana matumizi ya gharama za kampeni kwa kutofanya mikutano jimboni humo.
Kwa mujibu wa Mtenga, sheria ya uchaguzi inataka kampeni kufanyika ndani ya wakati uliopangwa na kwenye jimbo husika na si nje ya hapo.
Mtenga alisema CHADEMA jana ilifanya mikutano kwenye maeneo mbalimbali ya jimbo hilo kwa kutumia helikopta lakini mwitikio wa wananchi ulikuwa mdogo.
Katika hatua nyingine, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeponda uamuzi wa CHADEMA kutaka kuingiza jimboni humo watu 1,000 kwa ajili ya kulinda kura.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema vyama havina nafasi ya kulinda kura nje ya utaratibu.
Jaji Lubuva alisema vyama na wagombea wote wanapaswa kutii na kufuata utaratibu wa uchaguzi uliowekwa kisheria.
Alivitaka vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo na wagombea kuwa makini na kauli wanazotoa.
Mwakilishi wa CCM katika mkutano kati ya NEC na vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo, Miraj Mtaturu, alisema kauli ya Jaji Lubuva imetolewa wakati muafaka na itasaidia kufuatwa kwa utaratibu wa uchaguzi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru