Tuesday 4 March 2014

Nape: Maboresho daftari la kura hayana tija Kalenga

Na Mwandishi Wetu

KATIBU wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesema Chama hakiungi mkono hoja ya kutaka maboresho ya daftari la kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa Kalenga.
Amesema madai hilo halina tija na kamwe hayawezi kutekelezeka kutokana na kuwa muda ulibaki kupiga kura ni mdogo. Uchaguzi wa Kalenga unafanyika Machi 16, mwaka huu.

KATIBU wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye

Nape alisema hayo jana kuwa licha ya kuunga mkono maboresho hayo kwa ustawi wa demokrasia kitaifa, bado haafiki mantiki ya utekelezaji wake Kalenga katika kipindi kilichobakia uchaguzi kufanyika.
Alisema ugumu uliopo ni kwamba iwapo maboresho yatafanyika Kalenga, ina maana yatapaswa yafanyike katika maeneo mengine yenye uchaguzi mdogo, ikiwemo Chalinze na kata 27 zilikokuwa na uchaguzi mdogo, jambo ambalo halina tija kwa taifa.
“Tija hapa nina maana kukiwepo na ‘input’ (kinachoingizwa) iwe sawa na ‘output’ (kinachopatikana). Ukiwekeza sh. milioni 10, matunda yake yaendane na thamani yake,” alisema Nape katika ufafanuzi wa hoja yake.
Kwa mujibu wa Nape, mantiki nzuri na tija ya maboresho ya daftari la kupiga kura itakuwepo katika ngazi ya taifa, wakati kipindi cha uchaguzi mkuu kitakapowadia. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika mwakani.  
Alikanusha madai ya wapinzani kuwa upepo wa siasa unaielemea CCM  ndiyo maana inapinga maboresho hayo, badala yake ukweli ni kwamba neema ya ushindi iko kwa Godfrey Mgimwa, ambaye ndiye mgombea wa CCM. 
Nape alisisitiza kuwa hata katika tathmini ya kawaida ya hali inavyoendelea katika kampeni Kalenga, CCM inaungwa mkono kwa hali ya juu, hivyo hata kukiwepo maboresho ya daftari ya kupiga kura Kalenga yatakuwa ya manufaa zaidi kwa Chama chake.
Uchaguzi mdogo wa jimboni Kalenga, unafanyika baada ya kufariki kwa mbunge wake, Dk. William Mgimwa. 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru