Wednesday 12 March 2014

‘Rasimu ya kanuni imepita kwa mbinde’


NA EPSON LUHWAGO
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Ismail Jussa Ladhu, amesema kipindi cha kupitisha kanuni za bunge hilo kilijaa misukosuko na hata kuleta wasiwasi wa kutokufikiwa muafaka.
Jussa ambaye alikuwa mjumbe wa kamati ya kanuni iliyokuwa chini ya Profesa Costa Mahalu, alisema kuna wakati wajumbe wa kamati walikuwa wakikata tamaa kutokana na mwenendo ulivyokuwa ukiendelea.
Hata hivyo, alisema walipata faraja kutokana na utundu na ubunifu wa baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, ambao walifanya kazi ya ziada kuweka mambo sawa na hata kuweza kusonga mbele.
“Tulikuwa tunaona kama vile tunachokifanya hakina maana kwani mambo yalikuwa magumu sana. Lakini nimpongeze Tundu Lissu kwa ubunifu wake na umahiri katika kuweka sawa mambo,” alisema.
Pia, alisema wakati wa kufanya kazi hiyo, walikuwa wakitumiwa ujumbe na baadhi ya wajumbe wa bunge hilo na wananchi kutaka kuweka mambo wanayoyataka.
Alisema hali hiyo pia iliongeza ugumu kwa kuwa baadhi ya watu hao walikuwa wakitanguliza maslahi binafsi.
Hata hivyo, Jussa alisema kamati ya mashauriano iliyoundwa kuwaweka sawa wajumbe, imefanikisha kufikiwa kwa hatua ambayo imefikiwa hadi kukamilika kwa kanuni na kupitishwa na bunge.
Katika hatua nyingine, Jussa nusura achafue hali ya hewa baada ya kusema maslahi ya Zanzibar yatalindwa ndani ya kanuni pamoja na katiba mpya itakayoandaliwa.
“Mambo yote kuhusu Zanzibar yamezingatiwa. Nawahakikishia kuwa tuko tayari kulinda maslahi ya Zanzibar na hatutakuwa tayari kwa jambo ambalo litakuwa kinyume cha maslahi ya Zanzibar,” alisema.
Hatua hiyo iliwafanya baadhi ya wajumbe kuanza kumzomea kwa kuona kwamba alikuwa anataka kuonyesha upendeleo wa upande mmoja wa Muungano badala ya kuweka mbele maslahi ya taifa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru