Thursday 13 March 2014

Ofisa ya bunge yajivua madai ya madereva


NA CHARLES MGANGA, DODOMA
OFISI ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, imenawa mikono madai ya madereva wa wabunge la kutolipwa posho na kusema wanaopaswa kuulizwa ni wabunge na wajumbe wenyewe.
Katika taarifa yake jana, bunge lilisema halihusiki na malipo ya madereva na wasaidizi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini hapa kwa kuwa posho zao zimeanza kulipwa kupitia kwa wajumbe.
Kauli hiyo ya Bunge imekuja baada ya siku chache gazeti hili kuandika habari juu ya baadhi ya madereva wa wabunge kulalamikia kutokulipwa posho zao tangu kuanza kwa bunge maalumu la katiba kwa takriban wiki nne sasa. 
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema masharti yameainishwa na Rais Jakaya Kikwete kuhusu utaratibu wa malipo ya wajumbe hao wa Bunge la Katiba.
Alisema masharti yaliyowekwa ni kila mjumbe kupewa posho ya kujikimu ya sh. 230,000 kwa siku na kati ya hizo kuna sh. 45,000 za kuwalipa madereva wao kwa kila siku.
“Masharti yameainishwa wazi kuwa kila mjumbe atapaswa kulipwa fedha ya kujikimu kiasi cha sh. 230,000 na zile zingine za kikao ni sh. 70,000 kwa siku,” alisema.
Dk. Kashililah alifafanua kuwa masharti yaliwekwa hivyo kwa sababu baadhi ya wajumbe wengine hawana madereva, kwa maana kwamba wanajiendesha.
Hivi karibuni baadhi ya madereva wa wabunge, walilalamikia hatua ya kutokupewa posho zao tangu kuanza kwa Bunge Maalumu la Katiba wiki tatu zilizopita. 
Kutokana na hali hiyo, walidai kuwa wanaishi katika mazingira magumu ya kuwafanya wawe ombaomba au kuishi kwa kudra za Mungu.
Mbali na posho, madereva wengine walidai kuwa hawajalipwa hata mishahara yao na kuelezea kushangazwa na hatua ya mabosi wao kukaa kimya wakati uongozi wa bunge ulisema wanastahili kulipwa posho wakati wa bunge la katiba linaloendelea mjini hapa. 
Malalamiko hayo yalikuja siku chache baada ya Alhamisi iliyopita, wajumbe wa bunge maalumu la katiba kulipwa posho za siku 10 ambazo zilikuwa wastani wa sh. milioni tatu. 
Kila mmoja alilipwa kiwango cha posho kwa siku alizohudhuria vikao ambapo posho kwa siku ni sh. 300,000 kwa kila mjumbe.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru