Friday, 27 March 2015

Pengo amfikisha Gwajima polisi  • Ni kwa tuhuma za kumkashifu, kumtukana
  • Kova amtaka kujisalimisha haraka kituoni

NA MWANDISHI WETU
KIONGOZI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ameingia matatani na sasa ametakiwa kujisalimisha polisi kwa ajili ya kuhojiwa. 
Habari za kuaminika zinasema hatua ya Gwajima kutakiwa kujisalimisha polisi inatokana na tuhuma za kutoa matamshi ya kashfa dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Taarifa ya Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa vyombo vya habari jana, ilisema Gwajima anatakiwa kujisalimisha kutokana na tuhuma za kashfa na matusi.
Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema wamepokea malalamiko ya kukashfiwa na kutukanwa hadharani kutoka kwa Kardinali Pengo.
Alisema kupitia mitandao ya kijamii, kuna sauti na video zikimwonyesha Gwajima akimkashfu na kumtukana kwa maneno makali Kardinali Pengo, jambo ambalo limeonekana kuwaudhi wengi.
Kamishina Kova alisema baada ya tukio hilo, jitihada mbalimbali zimefanyika katika hali ya kawaida ili kumpata Gwajima bila mafanikio.
“Jitihada zimefanyika lakini hakuna mafanikio. Sasa tunamtaka ajisalimisha haraka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu bila kukosa na wala asisubiri kukamatwa,” alisema.
Alisema ni muhimu kwa Gwajima kuripoti mwenyewe badala ya kutafutwa au kukamatwa ili ajibu tuhuma hizo kutokana na nafasi yake katika jamii.
Kamishna Kova alisema tayari jalada la uchunguzi limefunguliwa na upelelezi kuhusiana na shauri hilo unaendelea ili sheria ichukue mkondo wake.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru